Na Linus R. James - MEATU DC
Mh Waziri wa Nchi OR-TAMISEMI , Mh. Suleiman Said Jaffo amesisitiza agenda ya kuleta mabadiliko kwa wananchi wa Meatu mapema leo akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Meatu.
“Wananchi walimchagua Mh. Dk. Magufuli kuwa Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili kuleta mabadiliko” Alisisitiza Jaffo.
Alisema kuwa ili kuleta mabadiliko katika sekta ya utumishi wa umma watumishi wanatakiwa kuondoa uzembe kazini na kushugulikia kero za wananchi.
“Fedha zinaweza kuja lakini zikikosa usimamizi hazitakuwa na maana na sisi watumishi ndio tumepewa dhamana ya kusimamia, sitaki watendaji wazembe katika ofisi yangu” alisisitiza.
Aliongeza pia kwa kutaja idara mbali mbali na kujaribu kuzikumbusha umuhimu wake katika kuleta mabadiliko kwa wananchi huku akikisisitiza suala la mipango mizuri ya Halmashauri, ukusanyaji mapato na tathimini ya utendaji kazi wa watumishi (OPRAS) huku akisisitiza Wahandisi wasimamie miradi vizuri na zabuni wapewe wakandarasi wenye uwezo.
Aidha Mh. Waziri amefafanua suala la kuipa halmashauri ya wilaya ya Meatu kipaumbele hasa kwenye sekta ya afya kwa kujitahidi kuwaletea miradi mingine ya vituo vya afya pamoja na kuongeza watumishi wengine.
Mapema akisoma taarifa ya mandeleo ya Wilaya ya Meatu, Mkurugenzi mtendaji Ndg. Fabian Manoza alibainisha changamoto mbali mbali zinazoikumba wilaya ya Meatu ikiwa ni pamoja na upungufu wa watumishi, madeni kwa watumishi, wakandarasi kutokuwa na uwezo katika miradi, pamoja na upungufu wa miundo mbinu ya afya.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Meatu Dk. Joseph Chilongani wakati akimkaribisha waziri alimwambia kuwa watumishi wana hamu kubwa ya kumuona hivyo anamshukuru sana kwa kupata nafasi ya kutembelea wilaya ya Meatu.
Ziara ya Mh. Jaffo ilianza kwa kutembelea mradi wa hospitali ya Wilaya ya Meatu huku akiambatana na viongozi mbali mbali amabao ni Mbunge wa Jimbo la Meatu M. Salum Khamis Salum, Mbunge Viti maalum, Mh. Leah Komanya , Viongozi wa CCM Mkoa na Wilaya pamoja na Viongozi wa mkoa wa Simiyu na Wilaya ya Meatu.
Mh Jaffo amehitimisha ziara wilayani Meatu kwa kusisitiza “Ndugu zangu, Ukitaka kuruka, agana na nyonga”. Huku akisisitiza kuwa mapungufu yote yaliyopo ndani ya Wilaya yatatuliwe haraka ili wilaya iendane na suala la mabadiliko.
MWISHO
Meatu, Simiyu, Tanzania
Anwani ya Posta: S.L.P 44
Simu: 028 2795 008
Simu ya Mkononi: 0622 404 712
Barua Pepe: ded@meatudc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Meatu . Haki Zote Zimehifadhiwa.