Kaimu Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Wilaya ya Meatu, Tibalilila Fabianus amewasilisha programu iitwayo TAKUKURU RAFIKI ambayo imebuniwa na kuzinduliwa na Taasisi hiyo hivi karibuni kwa lengo la kuwafikia wananchi katika maeneo yao na kusikiliza changamoto zinazowakabili.
Fabianus ameyasema hayo alipokaribishwa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Meatu muda mfupi baada ya kufungua kikao maalum cha Baraza la Madiwani ambacho kimefanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri ya Wilaya ya Meatu tarehe 27 Januari 2023 kujadili taarifa ya mapitio ya utekelezaji wa Mpango na Bajeti kwa mwaka wa fedha 2021/2022, nusu mwaka wa fedha 2022/2023 na mapendekezo ya Rasimu ya Mpango na Bajeti ya mwaka wa fedha 2023/2024.
"Tunafikiri changamoto zinazowakabili wananchi zisipotatuliwa zinaweza kusababisha vitendo vya rushwa hivyo kupitia programu hii tutaweka mikakati ya pamoja ya kutafuta ufumbuzi wa kuzitatua." Anasema Fabianus na kuongeza;
"Utekelezaji wa programu ya TAKUKURU RAFIKI utafanyika katika ngazibya kata kwa kuwashirikisha wadau mbalimbali kama vile Kamati za Maendeleo ya Kata- WDC's, Viongozi wa Dini na Wawakilishi wa Wananchi."
Fabianus amesema vitafanyika vikao ngazi kata ambapo Diwani wa Kata husika atakuwa Mwenyekiti, Mtendaji wa Kata atakuwa Katibu, Maafisa wa TAKUKURU watakuwa waratibu wa vikao hivyo na wadau wengine watakuwa Wajumbe.
Kaimu Mkuu huyo wa TAKUKURU amesema programu hiyo inatarajiwa kuanza utekelezaji wake mwezi Februari 2023 na ameomba ushirikiano wa viongozi hao katika maeneo yao.
Aidha, Baraza la Madiwani limeridhia na kupitisha Rasimu ya Mpango na Bajeti ya Halmashauri kwa mwaka wa fedha 2023/2024 ambapo imekadiria kukusanya na kutumia shilingi bilioni 39.97.
Kati ya fedha hizi Mapato ya Ndani ni shilingi bilioni 3.22 na kufanya ongezeko la asilimia 10 ukilinganisha na Bajeti ya mwaka 2022/2023 ambapo Bajeti ya Halmashauri ilikuwa shilingi bilioni 38.3.
Meatu, Simiyu, Tanzania
Anwani ya Posta: S.L.P 44
Simu: 028 2795 008
Simu ya Mkononi: 0622 404 712
Barua Pepe: ded@meatudc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Meatu . Haki Zote Zimehifadhiwa.