Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango amewaagiza Watendaji wa Kata na Viongozi wa Mikoa wa Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini - TARURA kutumia ipasavyo magari na pikipiki zilizonunuliwa na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR TAMISEMI) katika kuwafikia wananchi kwa urahisi, kuwasikiliza, kuwahudumia, kufuatilia utekelezaji wa miradi ya maendeleo na siyo kutumia kwa manufaa binafsi.
Makamu wa Rais ameyasema hayo wakati wa hafla ya kukabidhi magari 54 kwa TARURA pamoja na Pikipiki 916 kwa Watendaji Kata nchini katika hafla iliyofanyika kwenye Ukumbi wa Halmshauri ya Jiji la Dodoma, Mtumba tarehe 14 Februari 2023.
Halmashauri ya Wilaya ya Meatu katika mgao huo imepatiwa Pikipiki 9 ambazo zitagawiwa kwa Watendaji wa Kata wilayani humo.
Dkt. Mpango amewaagiza Watendaji hao kutambua na kushughulikia changamoto za wananchi kwa kuhakikisha vikao na wananchi katika ngazi ya Vijiji na Mitaa vinafanyika kwa mujibu wa Sheria.
Aidha, Makamu wa Rais amewaasa Watendaji wa Kata nchini kuacha mara moja uzembe wa kusimamia miradi ya maendeleo. Amesema utoaji wa vitendea kazi hivyo unalenga kuongeza ufanisi katika ufuatiliaji wa miradi pamoja na kufuatilia Uhifadhi wa mazingira kwa kutoa hamasa kwa Wananchi kupanda miti na kuimarisha shughuli za usafi wa mazingira ili kuwepo na maendeleo endelevu.
Dkt. Mpango amesisitiza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan itaendelea kuimarisha mfumo na utendaji wa Serikali za Mitaa, kwa kuzingatia misingi ya Kikatiba na Kisheria iliyopo kwani Serikali za Mitaa ndiyo njia pekee ya kusogeza huduma kwa Wananchi kwa kuwa unawashirikisha Wananchi katika kuamua, kupanga na kuchagua vipaumbele vya maendeleo yao na Taifa kwa ujumla.
Matukio katika Picha:
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango akimkabidhi pikipiki Afisa Mtendaji wa Kata ya Ng’ong’ona (wa pili kulia) iliyopo mkoani Dodoma kwa niaba ya Watendaji wengine wa Kata nchini ambao wamepata mgao wa Pikipiki 916. Pikipiki hizo zimenunuliwa na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR TAMISEMI) na kutolewa kwa Watendaji wa Kata nchini katika hafla iliofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Mtumba tarehe 14 Februari 2023. Wa kwanza kulia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Angellah Kairuki (Mb). (Picha zote na Ofisi ya Makamu wa Rais).
Meatu, Simiyu, Tanzania
Anwani ya Posta: S.L.P 44
Simu: 028 2795 008
Simu ya Mkononi: 0622 404 712
Barua Pepe: ded@meatudc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Meatu . Haki Zote Zimehifadhiwa.