Na Benton Nollo, MDC
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Dkt. Yahaya Nawanda ameitaka jamii kuendeelea kupinga mila potofu na kandamizi zinazorudisha nyuma juhudi za Mwanamke katika kufanya shughuli za kuleta Maendeleo.
Dkt. Nawanda amesema hayo wakati wa hotuba yake kwenye kilele cha maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani ambayo yamefanyika kimkoa mjini Mwanhuzi wilayani Meatu tarehe 08 Machi 2023.
"Nichukue nafasi hii kuwaomba akina baba tuendelee kushirikiana na akina mama na tuendelee kupinga mila zote ambazo zinamrudisha nyuma Mwanamke." Amesema Dkt. Nawanda.
Kwa upande wake Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Prisca Kayombo amemuahidi Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa Wanawake katika Mkoa wa Simiyu wataendelea kutekeleza majukumu yao yote kwa bidii ili kuleta chachu ya usawa wa kijinsia hasa katika uzalishaji wa bidhaa mbalimbali wanazozalisha akina mama.
Kadhalika, Mkuu wa Divisheni ya Maendeleo ya Jamii, Bonji Bugeni wakati akitoa maelezo mafupi kuhusu maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuwekeza nguvu kubwa kwenye sekta ya elimu hasa elimu kwa mtoto wa kike.
Bugeni amesema lengo la maadhimisho hayo ni kuikumbusha jamii juu ya mchango wa Wanawake katika jamii hususan kwenye nyanja za uchumi, afya, siasa, utamaduni, michezo na maendeleo ya kijamii kwa ujumla wake.
Ameongeza kuwa maadhimisho hayo pia, yanalenga kuongeza chachu katika harakati za kuleta usawa wa kijinsia kwa wanawake na wanaume katika jamii na kupunguza ama kuondoa mfumo dume kandamizi ambao hauthamini mchango wa wanawake katika jamii.
Bugeni amesisitiza na kuikumbusha jamii umuhimu wa elimu kwa wanawake na jamii kuongeza juhudi za kuandikisha watoto wa kike waliofikia umri wa kuanza shule za Awali na Msingi, kuwapeleka shule waliofanikiwa kujiunga na elimu ya Sekondari na vyuo vikuu.
Pia, Bugeni amewashukuru Wadau mbalimbali waliochangia rasilimali zao ili kufanikisha maadhimisho hayo ambapo aliwataja kuwa ni Mwiba Holdings Limited, NSSF, NMB Mwanhuzi, bIORE Meatu, TARURA Wilaya ya Meatu, RUWASA Wilaya ya Meatu, Vikundi vya Wanawake na Vijana, Watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Meatu na Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo.
Naye, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Meatu, Dkt. Hussein Kapaya wakati akisoma taarifa fupi ya Hospitali ya Wilaya ya Meatu kwa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Dkt. Yahaya Nawanda amesema kwa kipindi cha miaka miwili ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Hospitali hiyo imepata upendeleo mkubwa wa kupatiwa fedha shilingi milioni 820 kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ndani ya Hospitali ili kuboresha afya za wananchi wake wa wilaya ya Meatu na Watanzania kwa ujumla.
Ameitaja miradi hiyo kuwa ni ujenzi wa Jengo la Wagonjwa Mahututi (ICU) ambalo limejengwa kwa gharama ya shilingi milioni 250 ambapo jengo hilo lina uwezo wa kuhudumia Wagonjwa 10 mahututi kwa wakati mmoja. Jengo hilo limeshakamilika na vifaa tayari vimeshapokelewa Bandarini Dar es Salaam ili lianze kutumika.
Dkt. Kapaya amesema mradi mwingine ni Ununuzi wa Mashine Mpya ya Kisasa ya Mionzi (Digital X-Ray Mashine) kwa shilingi milioni 420. Mashine hiyo ina uwezo wa kuhudumia wagonjwa 250 hadi 300 kwa siku na tayari imeshasimikwa.
Mradi wa tatu katika Hospitali hiyo ni Ujenzi wa Wodi ya Wazazi inayojengwa kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) kwa gharama ya shilingi milioni 135 ambapo baada ya kukamilika utakuwa na vyumba vinne vya kujifungulia na uwezo wa kulaza wazazi 22 kwa wakati mmoja.
Meatu, Simiyu, Tanzania
Anwani ya Posta: S.L.P 44
Simu: 028 2795 008
Simu ya Mkononi: 0622 404 712
Barua Pepe: ded@meatudc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Meatu . Haki Zote Zimehifadhiwa.