Na Benton Nollo, Mwanhuzi
Mkuu wa Wilaya ya Meatu, Fauzia Ngatumbura ametoa wito kwa wazazi na walezi wilayani humo kuzuia ulemavu usio wa lazima kwa kuwapeleka watoto wenye umri chini ya miaka 5 kwenye vituo vya kutolea huduma za afya ili wapatiwe Chanjo ya Kuzuia Ugonjwa wa Kupooza (Polio).
Ngatumbura ameyasema hayo wakati wa uzinduzi wa Kampeni ya Kitaifa ya Utoaji wa Chanjo Dhidi ya Ugonjwa wa Polio mzunguko wa tatu, uliofanyika katika Hospitali ya WIlaya ya Meatu mapema leo tarehe 01 Septemba 2022.
“Tunaweza tukaua uchumi wa nchi au nguvu kazi kwa namna nyingi, hata wewe mama ambaye umezaa mtoto wako vizuri halafu ikatokea hujampa chanjo ya polio akapata ulemavu familia hiyo inaweza ikajikuta inaingia kwenye umaskini mkubwa kwa sababu muda mwingi utakuwa ni wa kumhudumia mtoto.” Anasema Ngatumbura na kuongeza;
“Tumeona maeneo mengine mama kazi yake haendi kulima haendi kufanya biashara, kazi yake ni kukaa na mtoto mlemavu ambaye ulemavu wake umesababishwa na ugonjwa wa Polio, wewe utakuwa kazi yako ni kumhudumia muda wote…wananchi tuzuie ulemavu wa watoto usio wa lazima, hatukatai yawezekana Mwenyezi Mungu anampa mtu ulemavu wa aina nyingine, lakini usiwe ni ulemavu unaotokana na kwamba mtoto wa Kitanzania kukosa Chanjo ya Polio.”
Ngatumbura amewahimiza Wananchi kuisemea chanjo hiyo inayotolewa kwa njia yam atone, maeneo yote ili wananchi wote wapeleke watoto wao kupata chanjo hiyo muhimu kwa watoto na amewahakikishia kuwa chanjo hiyo ni salama na ni kwa maslahi ya watoto wa Kitanzania.
Aidha, Ngatumbura amewahimiza wananchi wote kuwa mabalozi ili zoezi hilo liweze kufanikiwa katika malengo yaliyokusudiwa kwani taifa linalengo la kuwaweka watu wake salama baada ya kuwepo kwa dalili za ugonjwa huo katika nchi jirani.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Meatu, Msoleni Dakawa ametumia fursa hiyo kumpongeza na kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kwa kuwajali wananchi hasa katika suala zima la kulinda na kuboresha afya za wananchi anaowaongoza kwa kuwekeza fedha nyingi katika sekta hiyo muhimu nchini.
“Sisi Halmashauri ya Wilaya ya Meatu tupo tayari kuhakikisha zoezi hili linafanikishwa kwa zaidi ya asilimia 100, kwa sasabu tumeshajipanga vizuri…niwaombe sana viongozi wenzetu ambao wapo kwenye ngazi ya wananchi…tushirikiane kwa pamoja tuhamasishe wananchi wapeleke watoto wao kwenye vituo vya kutolea huduma vili waweze kupata chanjo hiyo ambayo ni muhimu sana.” Amesema Dakawa.
Awali, akitoa taarifa ya uzinduzi wa Kampeni hiyo kitaifa, Mkuu wa Divisheni ya Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe Wilaya ya Meatu, Dkt. Frank Mganga amesema katika mzunguko wa pili Halmashauri hiyo ilipokea dozi 132,600 kwa lengo la kuwafikia watoto chini ya miaka 5, 115,301 katika vituo vyote vya kutolea huduma za afya 53, vituo visaidizi 85 na huduma tembezi za nyumba kwa nyumba ambapo Halmashauri ilifanikiwa kuchanja watoto 139,953 sawa na asilimia 121.
Dkt. Mganga amebainisha kuwa katika mzunguko wa tatu ulioanza leo tarehe 01 hadi 04 Septemba 2022, Halmashauri imepokea chanjo 149,000 kwa lengo la kuchanja watoto 144,140, vibebea chanjo 216, mabango na vipeperushi 100 pamoja Reflector 100.
Kauli Mbiu ya Kampeni ya Chanjo ya Polio ni; Mpe Chanjo, Okoa Maisha ambayo inatekelezwa na Serikali kwa kushirikiana na wafadhili wa Shirika la Umoja wa Taifa Linalohudumia Watoto - UNICEF pamoja na Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) ambapo lengo likiwa kuokoa maisha ya watoto.
Matukio Katika Picha Wakati wa Uzinduzi wa Kampeni ya Kitaifa ya Utoaji wa Chanjo Dhidi ya Ugonjwa wa Polio Mzunguko wa Tatu ambayo Inafanyika kwa siku Nne (tarehe 01 hadi 04 Septemba 2022)
Meatu, Simiyu, Tanzania
Anwani ya Posta: S.L.P 44
Simu: 028 2795 008
Simu ya Mkononi: 0622 404 712
Barua Pepe: ded@meatudc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Meatu . Haki Zote Zimehifadhiwa.