Na Benton Nollo, Mwanhuzi
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Dkt. Yahaya Nawanda ametangaza mkoa huo kuwa Kinara na chachu ya mabadiliko katika mapambano dhidi ya maambukizi mapya ya VVU.
Nawanda amewataka viongozi katika ngazi zote za kiutawala mkoani humo, kwamba kupitia vikao vya kisheria na ziara mbalimbali, kuweka msisitizo kuhusu ushiriki wa wanaume katika kampeni isemayo "Mwanaume Kwanza Jali Afya Yako, Pima VVU" kwani Mkoa wa Simiyu unataka kuwa kinara na chachu ya mabadiliko na kuungana pamoja katika mapambano ya vita hiyo.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Wilaya ya Meatu, Fauzia Ngatumbura alipokuwa akisoma hotuba kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu wakati wa maadhimisho ya Siku ya UKIMWI Duniani ambayo huadhimishwa kila mwaka tarehe 01 Desemba ambapo kimkoa maadhimisho hayo yamefanyika wilayani Meatu kwenye Kituo Kuu cha Mabasi cha Mwanhuzi tarehe 01 Desemba 2022.
Ngatumbura amesema maadhimisho hayo hufanyika ili kufanya tathmini ya kuona ni jinsi gani janga la UKIMWI lilivyoleta na kuendelea kuleta athari kubwa kwa mtu mmoja mmoja, familia na taifa kwa ujumla.
"Siku hii inatumika kuhamasisha umma ni jinsi gani tunaweza kupambana au kuepuka maambukizi mapya ya VVU na UKIMWI." Amesema Ngatumbura.
Ngatumbura amefafanua kuwa kauli mbiu ya mwaka huu ambayo inasema "Imarisha Usawa" inasisitiza kuimalisha Usawa katika maeneo yote katika jitihada za kudhibiti UKIMWI kwa kuhakikisha hakuna vikwazo vya kiusawa hasa wa kijinsia na utoaji wa huduma kwa kuzingatia Haki za Binadamu kwa ujumla na kuzingatia Haki za Wanawake na Wanawake Vijana.
Mkuu huyo wa Wilaya amesema pamoja na kupata taarifa ya hali ya maambukizi ya VVU na UKIMWI katika maadhimisho hayo, ameona ni vema jamii ikatambua kuwa mapambano dhidi ya ugonjwa hatari wa UVIKO - 19 yanaendelea ambapo lengo la mkoa wa Simiyu lilikuwa kuchanja wananchi 1,010,011 lakini hadi kufikia tarehe 24 Novemba 2022 wananchi 1,041,753 sawa na asilimia 103 walikuwa wamepata chanjo ya UVIKO - 19.
Awali akisoma taarifa ya hali ya Maambukizi ya VVU/UKIMWI Mkoa wa Simiyu kwa niaba ya Katibu Tawala wa Mkoa huo, Mratibu wa UKIMWI Mkoa wa Simiyu, Dkt. Hamisi Kulemba amesema kwa mujibu wa utafiti wa matokeo ya ya Virusi vya UKIMWI na UKIMWI wa mwaka 2016 – 2017, kiwango cha maambukizi ya VVU katika Mkoa wa Sumiyu ni asilimia 3.9 chini ya kiwango cha kitaifa ambacho ni asilimi 4.7.
Dkt. Kulemba amefafanua kuwa kiwango cha maambukizi mapya kimeendelea kushuka mwaka hadi mwaka ambapo kwa mwaka 2019 wateja wapya waliogundulika kuwa na VVU walikuwa 6,836, mwaka 2020 walikuwa 6,440, mwaka 2021 walikuwa 6,029 wakati mpaka kufikia mwezi Oktoba 2022 wateja wapya waliogundulika kuwa na VVU ni 5,225.
Pia, Dkt. Kulemba amesema Mkoa wa Simiyu umeendelea kutekeleza na kusimamia shughuli mbalimbali katika Halmashauri zote kuhusu mikakati ya kupambana na maambukizi mapya ya VVU na UKIMWI matharani katika huduma za ushauri nasaha na upimaji mpaka kufikia mwezi Oktoba 2022 wateja 351,933 katika vituo 191 vya kutolea huduma za afya walipatiwa ushauri nasaha na upimaji sawa na asilimi 82.2 ya lengo la upimaji kwa mwaka 2022.
Kwa upande wa Huduma za Tohara Kinga kwa Wanaume, Dkt. Kulemba amesema mkoa kwa kushirikiana na Mdau ambaye ni Amref kupitia Mradi wa Afya Kamilifu umeendelea kutekeleza afua hiyo kwa lengo la kuzuia maambukizi mapya ya VVU ambapo tafiti zimeonesha kuwa Tohara Kinga kwa wanaume ina uwezo wa kuzuia maambikizi ya VVU kwa wananume kwa asilimia 60.
“Mheshimiwa Mgeni Rasmi katika utafiti wa mwaka 2016 – 2017 Mkoa wa wetu ulibainika kuwa na kiwango cha chini cha tohara kwa wanaume kwa asilimia 46 lakini kwa kipindi cha Januari hadi Oktoba 2022, wanaume 24,515 sawa na asilimia 46 ya lengo la mkoa walikuwa wamefikiwa na kupewa huduma ya tohara kinga na kufanya mkoa kufikia asilimia 76 ya Tohara kawa Wanaume.” Amesema Dkt. Kulemba.
Huduma za Tiba na Matunzo ni moja ya shughuli zilizotekelezwa na Mkoa ambapo Dkt. Kulemba amesema mkoa umeongeza vituo vya kutolea huduma hizo kutoka 106 mwaka 2021 hadi kufikia vituo 123 mwezi Septemba 2022. Ambapo katika kipindi cha Januari hadui Septemba 2022 watu 3,914 waliweza kupatiwa huduma za tiba na matunzo kwenye vituo vya kutolea huduma.
Aidha, Dkt. Kulemba amesema shughuli nyingine zilizosimamiwa ni huduma za Kufubaza Virusi Mwilini, huduma za Kifua Kikuu na UKIMWI pamoja na kuzuia Maambukizi ya VVU kutoka kwa Mama kwenda kwa Mtoto ambapo mkoa umepanga kuondoa kabisa au kutokomeza aina hii ya maambukizi.
Ambapo kwa kutekeleza azimio hilo, Dkt. Kulemba amesema mkoa kwa kipindi cha Januari hadi Septemba 2022 akina mama wajawazito 55,778 walipata huduma za ushauri nasaha na upimaji, kati yao 476 walibainika kuwa na maambukizi sawa na ushamiri wa asilimia 8.5. Aidha, akina mama 433 waliokuwa na maambukizi walianzishiwa dawa za kufubaza VVU ili kumkinga mama na mtoto.
Meatu, Simiyu, Tanzania
Anwani ya Posta: S.L.P 44
Simu: 028 2795 008
Simu ya Mkononi: 0622 404 712
Barua Pepe: ded@meatudc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Meatu . Haki Zote Zimehifadhiwa.