Na Benton Nollo, Bariadi.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Dkt. Yahaya Nawanda amemshukuru na kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuuwezesha mkoa huo kupata fedha za utekelezaji wa miradi ya maendeleo ikiwemo sekta ya maji.
Dkt. Nawanda ametoa shukrani hizo wakati akizungumza katika hafla fupi ya utiaji saini Mikataba ya Utekelezaji wa Miradi ya Maji mkoni humo kati ya Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini - RUWASA Mkoa wa Simiyu na Wakandarasi watakaotekeleza miradi hiyo, iliyofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Bariadi tarehe 11 Januari 2023.
Amesema katika sekta ya maji kwa mwaka wa fedha 2021/2022 mkoa huo ulipokea shilingi bilioni 22.5 kwa ajili ya miradi 36 na shilingi bilioni 1.9 za Mradi wa Kukabiliana na Tabia ya Nchi kwa ajili ya kuwalipa fidia Wananchi kupisha ujenzi wa miundombinu ya maji kutoka Ziwa Viktoria kwenda Wilaya za Busega, Bariadi na Itilima.
Mkuu huyo wa Mkoa amesema mikataba hiyo ina thamani ya shilingi bilioni 4.095 na itatekeleza miradi nane kati ya miradi 15 iliyotengewa shilingi bilioni 14.9 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya maji mkoani humo kwa mwaka wa fedha 2022/2023.
Dkt. Nawanda ametumia fura hiyo kuwapongeza Wataalam wa RUWASA ngazi ya mkoa na wilaya kwa kusimamia vema miradi ya maji mkoani humo.
Pia, Dkt. Nawanda ametoa rai kwa viongozi na watendaji wote waliohudhuria hafla hiyo kuwa wana wajibu wa kuhakikisha fedha zinazotolewa na Serikali zinasimamiwa vizuri na kwa wakati ili zilete tija kwa Wananchi ambao ndiyo walengwa na wanufaika wakubwa wa huduma ya maji.
Aidha, Dkt. Nawanda amewaonya Wakandarasi hao kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kwa wakati uliopangwa na si vinginevyo kwani Serikali imewaona wana sifa za taaluma na vifaa vyenye uwezo wa kukamilisha miradi hiyo kwa ubora.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Meneja Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini - RUWASA Mkoa wa Simiyu, Mhandisi Mariam Majala wakati wa hafla hiyo, amesema hali ya upatikanaji wa huduma ya maji wilayani Meatu mpaka kufikia mwezi Desemba 2022 ni asilimia 69.14 ya watu wanaopata huduma hiyo ambao ni 223,000 kati ya watu 322,525 wa Wilaya hiyo.
Wakandarasi waliosaini mikataba ya kutekeleza miradi hiyo ni URSINO Ltd ya Dar es Salaam, OTONDE Construction and General Supplies LTD ya Mwanza, MHAPA Builders and Road Works ya Shinyanga na JONTA Investment Ltd ya Shinyanga.
Wakandarasi wengine ni CORSYNE Consult Ltd ya Mwanza, EPIC Construction Limited ya Dar es Salaam, TRIBUTE ENERGEY Company LTD ya Dar es Salaam na DALEX BUILDING SERVICES COMPANY LTD ya Dar es Salaam.
Meatu, Simiyu, Tanzania
Anwani ya Posta: S.L.P 44
Simu: 028 2795 008
Simu ya Mkononi: 0622 404 712
Barua Pepe: ded@meatudc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Meatu . Haki Zote Zimehifadhiwa.