Benton Nollo, Meatu
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Meatu, Msoleni Dakawa amekikabidhi Kikundi cha Vijana cha The Heroes kilichopo Mwanhuzi, Basi aina ya Coaster lenye thamani ya shilingi milioni 62 katika hafla fupi iliyofanyika tarehe 20 Mei 2022 Makao Makuu ya Halmashauri hiyo.
Dakawa amekikabidhi kikundi hicho basi hilo lenye namba za usajili T 470 DZF baada ya kikundi hicho kupatiwa mkopo wa shilingi milioni 72 fedha ambazo ni asilimia 10 inayotolewa na Halmashauri hiyo kupitia mapato yake ya ndani kwa ajili ya mikopo ya Wanawake, Vijana na Wenye Ulemavu.
Bahi hilo la abiria litafanya safari zake kuanzia saa 04:00 asubuhi kutoka Meatu mjini (Mwanhuzi) kwenda Shinyanga na saa 10:00 jioni kutoka Shinyanga kurudi Meatu kila siku.
Kikundi hicho kimeanzishwa tarehe 29 Aprili 2019 kikiwa na wanachama watano (5) ambaowalikuwa wanajishughulisha na mradi wa pikipiki (bodaboda) za kuajiriwa.
Kikundi cha The Heroes kilisajiliwa rasmi tarehe 06 Mei 2020 na kutambulika kwa Namba ya Usajili MDC/IGA/Na. 13192.
Makao Makuu ya Kikundi cha The Heroes yapo Kijiji cha Bomani, Kata ya Mwanhuzi katika Tarafa ya Kimali ambapo kwa mara ya kwanza tarehe 15 Mei 2020 kilipatiwa mkopo wa shilingi milioni 2.5 ambazo zilitumika kununulia pikipiki moja kwa ajili ya shughuli za kusafirisha abiria maarufu kama bodaboda na kilitakiwa kurejesha fedha hizo ndani ya miaka miwili yaani miezi 24, lakini wanakikundi walifanikiwa kurejesha mkopo huo kwa muda miezi 11 tu.
Kwa awamu ya pili, tarehe 05 Aprili 2021 kikundi kilikopeshwa tena shilingi milioni 5 ambapo kikundi kilitumia mkopo huo kununua pikipiki nyingine mbili kwa ajili ya huduma hiyo hiyo ya usafirishaji wa abiria na kilipaswa kurejesha mkopo huo ndani ya miezi 24 lakini wanakikundi walifanikiwa kurejesha kwa miezi 10.
Baada ya kuonesha mafanikio makubwa hasa katika suala la uaminifu na urejeshaji wa mkopo kwa wakati, tarehe 10 Mei 2022 kikundi kimeomba na kupata mkopo wa shilingi milioni 72 ambazo kati yake shilingi milioni 62 zimetumika kununua basi hilo na fedha nyingine iliyobaki imetumika kama dharura na ukamilishaji wa taratibu nyingine za kisheria ikiwemo kulipia bima.
Pamoja na mambo mengine, kikundi hicho kimefanikiwa kutoa ajira kwa watu wanne ambapo watatu kati ya hao ni madereva wa pikipiki 3 na mmoja ni dereva wa basi hilo.
Kwa mwaka wa fedha 2021/2022, Kikundi cha The Heroes kinakuwa kikundi cha pili katika Halmashauri ya Wilaya ya Meatu kukopesha mkopo mkubwa baada ya kikundi cha awali cha Wanawake (Hapa Kazi Tu) cha Bukundi kukopeshwa shilingi milioni 74 ambazo nao wamezitumia kununua Trekta kwa ajili ya shughuli za kilimo na usafirishaji.
Aidha, Halmashauri ya Wilaya ya Meatu kwa kipindi cha Julai 2021 hadi Machi 2022 imetoa mikopo kwa vikundi 50 ambapo shilingi milioni 329.4 zimekopeshwa kwa vikundi vya Wanawake, Vijana na Wenye Ulemavu.
Muonekano wa Basi aina ya Coaster lililonunuliwa na Kikundi cha Vijana cha 'The Heroes' cha mjini Mwanhuzi baada ya kukopeshwa na Halmashauri ya Wilaya ya Meatu shilingi milioni 72 kupitia mikopo ya asilimia 10 ya Wanawake, Vijana na Wenye Ulemavu ambayo kwa mujibu ya sheria inatokana na mapato ya ndani ya Halmashauri.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Meatu, Msoleni Dakawa (aliyevaa koti la suti) akiwa katika picha ya pamoja na Wakuu wa Idara na Vitengo pamoja na watumishi mbalimbali baada ya kuwakabidhi Basi aina ya Coaster Kikundi cha Vijana cha 'The Heroes' cha mjini Mwanhuzi walilolinunua baada ya kukopeshwa na Halmashauri ya Wilaya ya Meatu shilingi milioni 72 kupitia mikopo ya asilimia 10 ya Wanawake, Vijana na Wenye Ulemavu ambayo kwa mujibu ya sheria inatokana na mapato ya ndani ya Halmashauri. (Picha zote na Benton Nollo).
Meatu, Simiyu, Tanzania
Anwani ya Posta: S.L.P 44
Simu: 028 2795 008
Simu ya Mkononi: 0622 404 712
Barua Pepe: ded@meatudc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Meatu . Haki Zote Zimehifadhiwa.