Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt. Laurian Ndumbaro amesema taarifa ya rufaa ya watumishi waliobainika kuwa na vyeti feki itatolewa Juni 30, mwaka huu, 2017.
Dkt Ndumbaro ameyasema hayo wakati alipozungumza na viongozi ngazi ya Mkoa na Wilaya, ambao ni wasimamizi wa Watumishi wa Umma Mkoani Simiyu katika kikao kilichofanyika Mjini Bariadi ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Wiki ya Utumishi nchini.
Amesema katika zoezi la uhakiki la awamu ya kwanza Watumishi zaidi ya 9,000 walibainika kuwa na vyeti feki ambapo kati yao ni asilimia kumi tu (10%) ndiyo waliokata rufaa.
“ Taarifa itawasilishwa tarehe 30 mwezi huu na baada ya kuwasilishwa kwa taarifa ya rufaa hizo maelekezo yatatolewa namna ya kuhitimisha ajira za watu wenye vyeti feki” amesema
Aidha, amesema baada ya taarifa ya rufaa kuwasilishwa Serikali itatangaza vibali vya nafasi za ajira kwa watumishi watakaojaza nafasi zitakazoachwa wazi na zile zilizotengwa.
Wakati huo huo Katibu Mkuu huyo amewataka viongozi wasisite kuwachukulia hatua watumishi wanaokiuka sheria, kanuni na taratibu za Utumishi wa Umma na kuwapongeza wanaofanya kazi kwa bidii ili kuwapa motisha.
“Kusiwe na masuala ya kuhamisha watumishi wanaosumbua, kama mtu anasumbua malizana naye pale pale fuata taratibu mfungulie mashtaka, ili tujenge utumishi wa Umma wenye uadilifu na weledi, lakini pia wale wanaofanya kazi vizuri wapongezeni mkiwaacha mtawakatisha tamaa” alisema.
Kuhusu suala la Watumishi kupandishwa vyeo Dkt.Ndumbaro amesema lifanyike kama motisha kwa watumishi wanaofanya kazi vizuri kwa kuzingatia ufanisi katika utendaji wa kazi,bajeti, masharti mengine ya upandaji vyeo kwa watumishi likiwepo la kufanya kazi kwa muda usiopungua miaka mitatu katika cheo kimoja.
Katika hatua nyingine Dkt. Ndumbaro amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri kuwasimamia Maafisa Utumishi wanaosimamia mfumo wa mshahara wa LAWSON kuhakikisha wanaunganisha taarifa za mfumo huo na takwimu za Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa NIDA kwa ufasaha na kuwakumbusha watumishi kuangalia taarifa zao ili wazihakiki ikiwa ziko sahihi na halali.
Akitoa shukrani kwa niaba ya Watumishi wa Umma mkoani Simiyu, Katibu Tawala Mkoa ameahidi kutekeleza na kuhakikisha watendaji wengine wanatekeleza maelekezo yote yaliyotolewa na Katibu Mkuu ili Utumishi wa Umma ufanyike katika maadili, ufanisi na weledi kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu.
Kwa Upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Itilima, Ndg.Mariano Mwanyigu ameshauri Serikali iangalie kwa upya umri wa kustaafu kwa hiari ambao ni miaka 55, kwa mujibu wa sheria miaka 60 na kuona uwezekano wa kupunguza miaka ili kutoa nafasi kwa vijana wengi walio nje ya mfumo kupata ajira.
Kikao hicho ambacho pia kimetumika kutoa taarifa, maagizo na maelekezo mbalimbali kimewashirikisha Makatibu Tawala Wasaidizi wa Sekretarieti ya Mkoa, Makatibu Tawala wa Wilaya,Wakurugenzi wa Halmashauri, Wakuu wa Idara na Vitengo wa Halmashauri na Maafisa Utumishi wanaoshughulikia Mfumo wa mshahara wa LAWSON.
Meatu, Simiyu, Tanzania
Anwani ya Posta: S.L.P 44
Simu: 028 2795 008
Simu ya Mkononi: 0622 404 712
Barua Pepe: ded@meatudc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Meatu . Haki Zote Zimehifadhiwa.