Mkoa wa Simiyu umezindua Mpango wa kupima maeneo ya wafugaji na wakulima kwa kutumia teknolojia ya kisasa ya ndege nyuki (drones) lengo likiwa ni kuwawezesha kuyatambua maeneo yao na kupewa hati miliki na baadaye kuyawekea miundombinu muhimu ya ufugaji na kilimo na kuondokana na migogoro kati ya wakulima na wafugaji.
Zoezi hilo limezinduliwa na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe. Anthony Mtaka katika kata ya Ng’hoboko wilayani Meatu na linatekelezwa Chini ya Serikali kwa Kushirikiana na Taasisi Ya Utafiti wa Masuala ya Kiuchumi na Kijamii (ESRF).
Amesema Mkoa huo ndiyo unaoongoza kwa kilimocha pamba nchini na ni miongoni mwa mikoa yenye ng’ombe wengi nchini, kwa kuwa wakulima na wafugaji wanamiliki ardhi ni vema maeneo yao yakapimwa wakapewa hati miliki na baadaye watalaam wa ardhi wawasaidie kuandaa mpango wa matumizi bora ya ardhi.
Ameongeza kuwa wafugaji wa mkoa wa Simiyu wamekuwa wakitozwa faini katika maeneo mbalimbali hivyo ili kuondokana na kadhia hiyo maeneo yao yakipimwa na wakaweka miundombinu muhimu kama vile mabwawa, visima, majosho na maeneo ya malisho wataondokana na uchungaji wa mifugo na kwenda kwenye ufugaji wenye tija
“Tungehitaji mpime mashamba yenu yakishapimwa mtapewa hati, watalaam wa halmashauri watawatengenezea mpango wa matumizi bora ya ardhi na kuwashauri namna sahihi ya uwekeaji wa miundombinu kama majosho, mabwawa, visima ili muwe wafugaji wenye tija ambao hamtapigwa faini wala kuibiwa ng’ombe” alisema.
Kwa upande wake Mkuu wa Mfumo kutoka Taasisi ya Utafiti wa Masuala ya Kiuchumi na Kijamii(ESRF) Bw. John Kajiba amesema upimaji kwa kutumia teknolojia ya ndege nyuki utafanyika kwa urahisi na haraka zaidi na ikilinganishwa na upimaji wa watu moja kwa kwa moja.
“Uzuri wa kutumia ndege nyuki ni kwamba tutatumia muda mfupi sana kupima eneo kubwa kwa wakati mmoja mfano, eneo ambalo lngeweza kupimwa na watu wane kwa muda wa siku nne drone(ndege nyuki) inafanya kwa muda wa siku moja” alisema.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Meatu, Mhe. Pius Machungwa amesema upimaji wa maeneo ya wakulima na wafugaji utawasaidia kutatua migogoro kati ya wakulima na wafugaji na kupata hati ziatazowasaidia kuchukua mikopo kwenye taasisi za kifedha na kufanya shughuli za maendeleo kupitia maeneo yao
Nao wananchi wa Meatu wanasema wameupokea mpango huo kwa mikono miwili kwa sababu watakuwa na uhakika wa umiliki wa maeneo yao baaada ya kupewa hati ambazo pia wamesema zitawasaidia kukopa mitaji ya kufuga na kulima kisasa na kwa tija.
“ Tumeupokea mradi huu kwa mikono miwili maana tutakapopimiwa maeneo yetu tutakuwa tunakopesheka kwenye taasisi za fedha, vile vile tutakuwa tumeondokana na migogoro kati ya wakulima na wafugaji kwa sababu maeneo yetu yatakuwa na mipaka iliyo wazi na kila mmoja atakuwa na hati ya kumili eneo lake” alisema John Mchagula mfugaji kutoka Kijiji cha Ng’hoboko
Meatu, Simiyu, Tanzania
Anwani ya Posta: S.L.P 44
Simu: 028 2795 008
Simu ya Mkononi: 0622 404 712
Barua Pepe: ded@meatudc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Meatu . Haki Zote Zimehifadhiwa.