Mwenyekiti wa Timu maalum ya mawaziri wanane ya kupitia maeneo yenye migogoro kati ya wananchi na maeneo ya Hifadhi ambaye ni Waziri wa Ardhi,Nyumba na Maendeleo na Makazi Mhe. Wiliam Lukuvi amepokea ombi la wananchi wa wilaya tatu za mkoa wa Simiyu wanaoishi katika vijiji vinavyopakana na Pori la akiba la Maswa la kupewa eneo lenye urefu wa kilometa kumi, kwa ajili ya malisho na kuahidi kulifikisha kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kwa hatua zaidi.
Mhe. Lukuvi ameyasema hayo jana wakati akizungumza na wananchi wa vijiji vinavyopakana na pori la akiba la Maswa katika mkutano wa hadhara uliofanyika Mji mdogo wa Mwandoya wilayani Meatu.
Awali akijibu baadhi ya kero zilizowasilishwa na Mwananchi wa Wilaya ya Meatu, Bw. Deusdedith Martin Waziri Lukuvi amesema timu hiyo imezisikia kero hizo na akaahidi kuwasilisha taarifa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli na kubainisha kuwa taarifa rasmi ya majibu ya kero zao itatolewa.
Aidha, Waziri Lukuvi amewahakikishia wananchi kuwa zoezi la kupima eneo la mita 500 kutoka kwenye mpaka wa Pori la Akiba la Maswa kuelekea kwenye vijiji vinavyopakana na Pori hilo (Buffer zone) katika Wilaya za Meatu, Itilima na Maswa limesimamishwa mpaka litakapotolewa maelekezo.
“Hapa kulikuwa na zoezi la kupima mita 500 kutoka kwenye mpaka wa Pori la Akiba la Maswa kuingia kwa wananchi, maana yake ni kwamba kuna wananchi wengi na vijiji vingi vingeathirika ili vipishe ‘buffer zone’, ingawa ni kwa mujibu wa sheria lakini ‘buffer zone’ ile ingekula maeneo ya vijiji kwa hiyo zoezi hilo limesimamishwa”
“Zoezi hili limesimamishwa kwa mujibu wa maelekezo ya Mhe Rais baada ya kuona watu wengi maskini ambao walipaswa kupisha maeneo ya hifadhi;...... vile vile kuanzia sasa zoezi lolote la kutambua mipaka litakalofanywa na watu wa Maliasili ni lazima liwe shirikishi” alisema Waziri Lukuvi.
Awali akiwasilisha taarifa kwa niaba ya wananchi wa Wilaya ya Meatu, Bw. Deusdedit Martin aliomba Timu ya Mawaziri wanane kuwasaidia katika kutatua changamoto ya ubadilishaji wa mpaka kati ya Pori la Akiba la Maswa na Vijiji vinavyopakana, Uvamizi wa tembo katika mashamba na makazi ya watu na kukatazwa kwa wananchi kulima katika eneo la mita 60 kutoka kwenye kingo za mito.
Kwa upande wake Waziri wa Maji, Mhe. Prof. Makame Mbarawa amewahakikishia wananchi wa Mkoa wa Simiyu upatikanaji wa uhakika wa maji kupitia mradi mkubwa wa Ziwa Victoria, ambapo amesema kwa sasa mradi upo katika hatua ya kumtafuta mkandarasi
Naye Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe.Omari Mgumba akieleza kuwa Serikali imejipanga kuhakikisha inatoa viatiifu kwa wakulima ambapo amesema hadi sasa zaidi ya chupa milioni saba zimeshasambazwa kwa wakulima katika mikoa inayolima pamba hapa nchini.
Timu ya Mawaziri wanane inayoongozwa na Waziri Lukuvi pia inajumuisha mawaziri kutoka Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Maliasili na Utalii, Mifugo na Uvuvi, Ofisi ya Rais TAMISEMI, Wizara ya Maji na Manaibu Waziri kutoka Wizara ya Kilimo na Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira.
Mwisho
Meatu, Simiyu, Tanzania
Anwani ya Posta: S.L.P 44
Simu: 028 2795 008
Simu ya Mkononi: 0622 404 712
Barua Pepe: ded@meatudc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Meatu . Haki Zote Zimehifadhiwa.