Na Benton Nollo, Mwanhuzi
Mkuu wa Wilaya ya Meatu, Fauzia Ngatumbura amewaagiza Watendaji wa Kata zote wilayani humo kusimamia na kulipa kipaumbele suala la Wanafunzi wa Darasa la Awali na Wanafunzi wa Kidato cha Kwanza kuripoti shuleni haraka iwezekanavyo.
Ngatumbura ametoa agizo hilo wakati wa kikao cha Wadau wa Uhifadhi kwa ajili ya Uandaaji wa Mpango wa Jumla wa Usimamizi wa Matumizi ya Rasilimali za Jumuiya ya Wanyamapori Makao kilichofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri ya Wilaya ya Meatu tarehe 24 Januari 2023.
"Mpaka sasa takriban wanafunzi wa Kidato cha Kwanza 1,756 hawajaripoti shuleni kuanza masomo...nitachukua hatua kwa Watendaji wa Kata na Vijiji ambao mpaka kufikia tarehe 30 Januari 2023 kutakuwa na Mwanafunzi ambaye hajaripoti shuleni...tukumbuke suala la Wanafunzi kwenda shule ni la lazima siyo hiari." Anasema Ngatumbura na kuongeza;
"Pia, ninawaagiza Watendaji wa Kata wote kusimamia suala la utoaji wa chakula shuleni kwani jambo hilo lina nafasi kubwa sana katika maendeleo ya Wanafunzi shuleni."
Halmashauri ya Wilaya ya Meatu ailpokea fedha kutoka Serikali Kuu shilingi bilioni 1.48 ili kujenga vyumba vya madarasa 74 kwa ajili ya Wanafunzi wa Kidato cha Kwanza mwaka 2023 ambapo madarasa hayo tayari ujenzi wake ulishakamilika na yameanza kutumika mhula wa masomo uliofunguliwa tarehe 09 Januari 2023.
Meatu, Simiyu, Tanzania
Anwani ya Posta: S.L.P 44
Simu: 028 2795 008
Simu ya Mkononi: 0622 404 712
Barua Pepe: ded@meatudc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Meatu . Haki Zote Zimehifadhiwa.