Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Tulia Ackson ametoa wito kwa wananchi kutobeza ngoma za asili na michezo na badala yake waone fursa zilizopo katika Michezo na Utamaduni ili ziweze kuwanufaisha.
Dkt. Tulia ameyasema hayo Julai 08, wakati akizungumza na wananchi wa Mkoa wa Simiyu katika Tamasha la SIMIYU JAMBO FESTIVAL Mjini Bariadi, ambalo limehusisha mashindano ya ngoma za asili (Wagika na Wagalu), mbio za baiskeli(Kilomita 150 wanaume na kilomita 100 wanawake), mbio fupi(Kilomita 10 na Kilomita tano), uandishi wa insha, likiwa limeshirikisha washiriki kutoka mikoa mbalimbali hapa nchini, nchi jirani ya Kenya.
Amesema wapo watu wengi amabao wamepata fursa ya kusafiri kwenda maeneo mbalimbali hapa dunia na kujipatia fedha kutokana na ngoma asili zinazotambulisha utamaduni wa makabila yao pamoja na michezo mbalimbali hivyo maeneo hayo hayatakiwi kubezwa.
“Niwaombe ndugu zangu isitokee mtu yeyote akafikiri ngoma za asili au michezo ni vitu vya kubeza, haya ni mambo ambayo kama nchi tumekuwa nayo na tunataka kuendelea nayo, wapo watu wametembea nchi nyingi duniani kwa sababu ya ngoma za asili na michezo, tuendelee kuunga mkono juhudi zinazofanywa kuendeleza michezo na utamaduni” alisema.
Akizungumzia kauli mbiu ya SIMIYU JAMBO FESTIVAL mwaka 2018 inayosema Familia Yangu, Furaha Fangu, Afya Yangu amepongeza ubunifu wa mkoa wa Simiyu kuja na kauli mbiu hiyo ambayo inatoa hamasa kwa wananchi kuona umuhimu wa kuthamini afya zao na akalishukuru Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia idadi ya watu Duniani(UNFPA) kwa kuboresha miundombinu ya Afya katika Mkoa huo.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka amesema mkoa wa Simiyu utabaki kuwa kielelezo katika Utamaduni huku akibainisha kuwa wamedhamiria kuufanya (kuuza) utamaduni wa mkoa huo ambao watu hucheza ngoma za asili na wanyama kama nyoka na fisi ili wananchi waweze kuona kunufaika na utamaduni wao.
Mhe. Mtaka amewashukuru wadhamini wa SIMIYU JAMBO FESTIVAL mwaka 2018 kwa namna walivyofanikisha, ambapo amesema mwaka huu wigo wa tamasha hilo umepanuliwa kwa kuongeza mashindano ya mbio fupi, uandishi wa insha tofauti na mwaka 2017 ambapo kulikuwa na mashindano ya mbio za baiskeli na ngoma za asili(Wagika na Wagalu)
Ameongeza kuwa amesema matarajio yake ni kuona mkoa wa Simiyu na Tanzania kwa ujumla inatoa wachezaji wa mchezo wa Mbio za baiskeli katika mashindano ya Olimpiki mwaka 2020, kupitia mashindano ya michezo mbalimbali iayofanyika katika Simiyu Festival.
Naye Mdhamini Mkuu wa Simiyu Jambo Festival mwaka 2018 Mhe. Salum Khamis mmiliki wa Jambo Food Products amesema kampuni yake itaendelea kudhamini tamasha hilo ambapo ameahidi kuwa mwaka 2019 itaongeza zawadi kutoka milioni 25 mwaka 2018 na kufikia milioni 35.
Kwa upande wao wananchi wa mkoa wa Simiyu wamesema Tamasha la Simiyu Jambo Festival mwaka 2018 limefana, limechangia kwa kiasi kikubwa kuutangaza Mkoa wa Simiyu hasa kupitia utamaduni wa Wagika na Wagalu na mchezo wa baiskeli na kusaidia kuchangia uchumi wa watu wa Simiyu.
“Yaani leo mji wa Bariadi wote umesimama kwa sababu ya tukio hili ambalo kwa mwaka huu limekuwa kubwa zaidi ya mwaka jana, halafu hata wafanyabishara wa Bariadi wamenufaikakupitia tukio hili, tumuombe Mkuu wetu wa mkoa aendelee kutuletea mambo yenye manufaa kwa wananchi wake.
Tamasha la Simiyu Jambo Festival mwaka 2018 lilishirikisha washiriki kutoka mikoa 13 hapa nchini na nchi jirani ya Kenya huku likihusisha mashindano ya mbio za baiskeli (kilomita 150 wanaume, kilomita 100 wanawake, kilomita 10 walemavu), mashindano ya mbio fupi(kilomita 10 na kilomita tano), mashindano ya ngoma za asili(Wagika na Wagalu) na mashindano ya uandishi wa insha kwa wanafunzi wa shule za sekondari.
Katika mashindano ya Mbio za Baiskeli wanaume kiliometa 150 Richard Laizer kutoka Arusha cha alishika nafasi ya kwanza na kujinyakulia kitita cha shilingi milioni 1.2 aliyekimbia Kilometa 150 na kwa uapnde wa wanawake Laulensia Ruzuba kutoka Mwanza aliyekimbia km 100 kwa dakika 3:06:20 aliibuka mshindi wa kwanza na kujipatia shilingi 1,000,000/=
Mkoa wa Simiyu pia ulifanya vizuri ambapo mchezaji wake Elizabeth Mwinamila ambaye alikimbia Km 100 kwa saa 3:10:58 alipata kiasi cha Sh. 800,000 akifuatiwa na Sophia Adson kutoka Arusha ambaye alikimbia kwa saa 3:15:47.
Kwa upande wa mbio fupi kilometa 10 Mshindi wa kwanza wanawake Esther Chesenga na wanaume Joseph Mbatha kutoka nchini Kenya walijinyakulia kitita cha shilingi 1,000,00/= na nafasi ya pili kwa wanaume ilichukuliwa na Fabian Sulle huku wanawake ikichukuliwa na Failuna Matanga
Simiyu Jambo Festival imefanyika kwa mara ya pili sasa mkoani Simiyu na litakuwa likifanyika kila mwaka likiwa ujumbe tofauti wa kufikisha kwa jamii.
Meatu, Simiyu, Tanzania
Anwani ya Posta: S.L.P 44
Simu: 028 2795 008
Simu ya Mkononi: 0622 404 712
Barua Pepe: ded@meatudc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Meatu . Haki Zote Zimehifadhiwa.