Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya CCM Taifa, Dkt. Edmund B. Mndolwa aliwaongoza viongozi wa CCM Taifa na Mkoa wa Simiyu na Shinyanga, pamoja na viongozi wa Serikali Mkoa wa Simiyujana katika kijiji cha Zebeya wilayani Maswa kwenye mazishi ya aliyekua diwani wa kata ya Tindabuligi wilaya ya Meatu marehem Seleman Mahega.
Akizungumza kwa niaba ya Mwenyekiti wa CCM Taifa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, Dkt. Mndolwa ametoa pole kwa familia ya marehemu Mahega na akawaomba ndugu na familia kuwa na subira katika kipindi kigumu walichonacho.
Amesema Mhe. Rais anatoa shukrani kwa Kituo cha Afya Mwandoya, Hospitali Teule ya Mkoa wa Simiyu, Hospitali ya Rufaa Bugando na Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa namna walivyowahudumia majeruhi 19 wa ajali hiyo ambapo baadhi yao walitibiwa na kuruhusiwa na wengine bado wanaendelea kupata matibabu.
Aidha, Dkt. Mdolwa amemshukuru Mbunge wa Kisesa ambaye pia ni Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Luhaga Mpina kwa kuchukua maamuzi ya haraka ya kukodi ndege iliyowapeleka majeruhi tisa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, kwa ajili ya matibabu na uchunguzi zaidi.
Naye mwenyekiti wa UVCCM Mh Kheri James amabaye ndiye alikua katika msafara wakati ajali ilipotokea alipataa nafasi ya kutoa salamu zamwisho
“Ndugu yangu aliyelala mbele yetu hapa, alinipokea mimi akanishika mkono na akaniambia mwenyekiti tumejiandaa kukupokea, Itilima hawawezi kutufunika sikujua kama Itilima walikua hawawezi kutufunika kwa staili hii, wala sikujua kwamba zile zilikua ni salamu za kuniaga na kuniambia kwamba mapokezi yale hayatakua mapokezi tena baada ya hapo” Alisema James wakati akitoa salamu za mwisho
“Nilitegemea atashirikiana na wajumbe wenzake wa halmashauri kuu ya CCM kunieleza chama kinaendeleaje kwenye wilaya yao, nlitegemea nitashirikiana naye na viongozi kuona tunafanyaje katika vikao vya serikali na chama kuona serikali nafanyaeje kufikia malengo yetu” alisistiza James huku baadhi ya waombolezjii wakilengwa na machozi.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka akitoa pole kwa familia, ndugu na Baraza la Madiwani Meatu amewashukuru viongozi wa Chama na Serikali ambao wametoa misaada mbalimbali katika kuhakikisha majeruhi wa ajali wanapata matibabu kwa wakati na marehemu anasitiriwa kwa heshima zote kama kiongozi.
Katika hatua nyingine Mtaka amemtaka Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Meatu kuhakikisha kuwa stahili zote za kisheria ambazo familia ya marehemu inapaswa kupewa na Halmashauri, zitolewe mapema badala ya kusubiri kufuatwa na familia hiyo.
Naye Waziri wa Mifugo na Uvuvi ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Kisesa iliko kata aliyokuwa anaitumikia marehemu Mahega amewashukuru viongozi wa Chama na Serikali kwa namna walivyojitoa katika kushughulikia majeruhi na msiba ambapo pia amewashukuru wananchi wa Wilaya ya Meatu na Maswa mahali alikozikwa marehemu kwa ushirikiano na upendo mkubwa waliounesha katika msiba huo tangu siku Mhe. Mahega alipofariki mpaka kuzikwa kwake.
Mpina ametoa pole kwa familia, wananchi wa kata ya Tindabuligu na Wilaya ya Meatu kwa ujumla kwa kuondokewa na Mhe. Mahega ambaye amesema ameacha pengo kubwa kwa kuwa alikuwa na mchango mkubwa katika maendeleo ya wananchi na Meatu kwa ujumla.
Kwa upande wake Diwani wa Viti maalum Mhe. Avelina Kyakwambala ambaye amefanya kazi na Marehemu kama madiwani toka mwaka 2000 , amesema msiba huo umeupokea kwa masikitiko makubwa na kwamba Meatu imepoteza diwani mwadilifu, mchapakazi, anayezingatia kanuni zote za baraza, chama chake na alikuwa tayari kukosoa na kukosolewa kwa ajili ya kujenga na kuleta maendeleo kwa wananchi.
Msiba wa Marehemu Mahega Selemani ambaye ameacha mke na watoto 14, umehudhuriwa na Wajumbe wa Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Viongozi wa CCM Mkoa wa Simiyu, Simiyu na Mwanza na Viongozi wa Serikali Mkoa wa Simiyu na wilaya zote mkoani humo
Meatu, Simiyu, Tanzania
Anwani ya Posta: S.L.P 44
Simu: 028 2795 008
Simu ya Mkononi: 0622 404 712
Barua Pepe: ded@meatudc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Meatu . Haki Zote Zimehifadhiwa.