Akizungumza kwenye siku ya uzinduzi wa msimu wa ununuzi wa pamba 2017/18 uliofanyika katika kijiji cha Mwabusalu Wilayani Meatu, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Zainab Telack alisema bei ya kilo moja ya pamba kwa msimu huu imepanda kutoka Sh. 1,000/= mwaka jana hadi Sh. 1,200/=.
Telack aliwaonya wakulima wa pamba kote Nchini kuacha kuchanganya maji, mawe na mchanga kwa ajili ya kuongeza uzito katika kipimo kwa kuwa watakaobainika watachukuliwa hatua za kisheria.
Aidha, alisema kuwa kufanya hivyo kunapunguza thamani ya zao hilo na kusababisha bei kushuka kwenye soko la dunia. “Serikali imejipanga kuhakikisha inawakamata na kuwachukulia hatua wale wote watakaobainika kuchafua pamba, ni vyema kuhakikisha mnavuna na kuuza pamba safi,” alisema Telack.
Pia aliwataka wanunuzi kuhakikisha mizani wanayotumia iwe imehakikiwa na wataalam wa vipimo ili wasiwaibie wakulima na kwamba watakaobainika watachukuliwa hatua za kisheria ikiwamo kuhukumiwa papo hapo na Mahakama inayotembea.
Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Pamba Tanzania (TCB) Marko Mtunga alisema wanatarajia kununua tani milioni moja za pamba nchi nzima.
“Matarajio hayo ni baada ya kuona uzalishaji kushuka kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa, pia kwa kuwa wakulima walikuwa wamekata tamaa ya kuzalisha” alisema. Kauli mbiu katika sherehe hizo za ufunguzi wa msimu ilikuwa; “Wekeza katika Kilimo cha Mkataba na Mbegu Bora kuelekea Tanzania ya Viwanda”
Meatu, Simiyu, Tanzania
Anwani ya Posta: S.L.P 44
Simu: 028 2795 008
Simu ya Mkononi: 0622 404 712
Barua Pepe: ded@meatudc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Meatu . Haki Zote Zimehifadhiwa.