Na Benton Nollo, Meatu
Halmashauri ya Wilaya ya Meatu, imeshika nafasi ya pili katika Mkoa wa Simiyu na nafasi ya 59 kwa Halmashauri zote nchini kwenye ukusanyaji wa mapato ya ndani kwa kigezo cha asilimia ya makusanyo kwa mwaka wa fedha 2021/2022.
Kwa mujibu wa taarifa ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serkali za Mitaa, Innocent Bashungwa (Mb) (pichani katikati) kuhusu Mapato na Matumizi ya Mapato ya Halmashauri zote 184 nchini kwa mwaka wa fedha 2021/2022 aliyoisoma jijini Dar es Salaam tarehe 02 Agosti 2022, imeainisha kwamba Halmashauri hiyo kwa kipindi cha mwaka husika ilipanga kukusanya shilingi bilioni 2.574 kupitia mapato yake ya ndani ambapo hadi kufikia mwezi Juni 2022 imefanikiwa kukusanya shilingi bilioni 2.745 sawa na asilimia 107.
Uchambuzi unaonesha kwamba, mwenendo wa ukusanyaji wa mapato ya ndani kwa kipindi cha Julai 2021 hadi Juni 2022, Halmashauri ya Wilaya ya Meatu ni miongoni mwa Halmashauri 100 nchini zilizokusanya mapato yake kwa zaidi ya asilimia 100.
Aidha, Halmashauri ya Wilaya ya Meatu imeshika nafasi ya pili katika Mkoa wa Simiyu na nafasi ya 42 katika ukusanyaji wa mapato ya ndani kwenye kundi la Halmashauri za Wilaya kuanzia Julai 2021 hadi Juni 30, 2022 kwa kigezo cha asilimia ya makusanyo.
Kwa upande wa matumizi ya mapato ya ndani kwenye miradi ya maendeleo kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2021/2022, Mapato yaliyokusanywa yasiyofungwa (Unprotected Revenue) katika Halmashauri ya Wilaya ya Meatu yalikuwa shilingi bilioni 2.324 ambapo fedha zilizopaswa kutumika kwenye miradi ya maendeleo ni shilingi milioni 929.713 ilhali fedha zilizotumika ni shilingi milioni 872.202 sawa na asilimia 38 na ambapo katika Mkoa wa Simiyu imeshika nafasi ya kwanza na nafasi ya 63 kati ya Halmashauri 184 nchini.
Halmashauri ya Wilaya ya Meatu katika mikopo ya asilimia 10 kwa mwaka wa fedha 2021/2022 kutokana na mapato yake ya ndani iliyokusanya (shilingi bilioni 2.324) ilifanikiwa kupeleka shilingi milioni 218.064 kwa ajili ya vikundi vya Wanawake, Vijana na Wenye Ulemavu sawa na asilimia 9 ya mapato husika na hivyo kushika nafasi ya pili katika Mkoa wa Simiyu na nafasi ya 55 katika Halmashauri 184 nchini.
Kadhalika, utekelezaji wa Hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka wa fedha 2021/2022, Halmashauri ya Wilaya ya Meatu ilikuwa na Hoja 95 ambapo zilizojibiwa na kufungwa ni 55 sawa na asilimia 57.9 ambapo katika alama 20 Halmashauri ya Wilaya ya Meatu ilipata alama 11.6 na kushika nafasi ya pili kimkoa na nafasi ya 66 katika ya Halmashauri 184 Tanzania Bara.
Pamoja na mambo mengine, kuhusu utoaji wa mrejesho na uhabarishaji Wananchi kwa kipindi cha kuishia Mwezi Juni 2022, Halmashauri ya Wilaya ya Meatu ilishika nafasi ya 165 katia ya Halmashauri 184.
Kuhusu Tathmini ya jumla ya Utendaji wa Haslmashauri kwa kipindi cha kuanzia mwezi Julai 2021 hadi Juni 2022, Halmashauri ya Wilaya ya Meatu imepata alama 77.8 ambalo ni Dalaja B+ na kushika nafasi ya pili katika Mkoa wa Simiyu na nafasi ya 64 katika Halmashauri 184 nchini.
(Chanzo: Ni taarifa ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, Innocent Bashungwa (Mb) kuhusu Mapato na Matumizi ya Mapato ya Ndani ya Halmashauri kwa mwaka wa fedha 2021/2022 aliyoisoma katika Mkutano wake na Waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam tarehe 02 Agosti 2022.)
Meatu, Simiyu, Tanzania
Anwani ya Posta: S.L.P 44
Simu: 028 2795 008
Simu ya Mkononi: 0622 404 712
Barua Pepe: ded@meatudc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Meatu . Haki Zote Zimehifadhiwa.