Katibu Tawala Mkoa wa Simiyu, Ndg.Jumanne Sagini amewataka Wakurugenzi Watendaji wa Halmashauri Mkoani Simiyu kuandaa Mipango Mikakati katika Halmashauri zao.
Sagini ameyasema hayo wakati akifungua mafunzo ya siku tatu ya uandaaji wa Mipango mikakati ya Mamlaka za Serikali za Mitaa Mkoani Simiyu yanayofanyika wilayani Busega, chini ya Mpango wa Maboresho ya Usimamizi wa Fedha za Umma katika Mamlaka za Serikali za Mitaa (PFMRP).
Amesema wakurugenzi wote wahakikishe wanatumia rasilimali zilizopo katika maeneo yao kuhakikisha kuwa wanakamilisha uandaaji wa mipango mikakati hiyo.“ Niwaombe Wakurugenzi Watendaji kuepuka visingizio vya kutokuwa na fedha kutekeleza jambo hili na badala yake mjipange kwa kutumia rasilimali tulizonazo” amesema.
Aidha, amesema Mpango Mkakati ni muhimu kwa kila Halmashari kwa kuwa unasaidia Halmashauri kufikia malengo ya kuanzishwa kwake na kuboresha utoaji huduma za kiuchumi na kijamii kwa wananchi.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi, Ndg.Abdallah Malela amesema mafunzo hayo yatawasaidia wao kama viongozi na watendaji wengine katika Halmashauri zao kutekeleza shughuli mbalimbali za maendeleo zikiwemo za uanzishwaji na uendeshaji wa viwanda kimkakati.
Wakati huo huo Katibu Tawala huyo amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri kuendelea kutenga maeneo ili kuwezesha utekelezaji wa Sera ya Ujenzi wa Uchumi wa Viwanda Mkoani Simiyu.
Mafunzo ya uandaaji wa Mipango mikakati ya Mamlaka za Serikali za Mitaa (Halmashauri) yamewahusisha Wakurugenzi, Wataalam wa Idara ya Kilimo, Fedha, Mipango na Maendeleo ya Jamii kutoka Halmashauri zote sita za Mkoa huo (Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi, Busega, Itilima, Maswa, Meatu na Halmashauri ya Mji Bariadi).
Meatu, Simiyu, Tanzania
Anwani ya Posta: S.L.P 44
Simu: 028 2795 008
Simu ya Mkononi: 0622 404 712
Barua Pepe: ded@meatudc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Meatu . Haki Zote Zimehifadhiwa.