Katibu Makuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhandisi Mussa Iyombe ameziagiza Halmashauri zote nchini kuhakikisha wanajitathmini katika utendaji kazi wao hususani katika kuihudumia jamii.
Mhandisi Iyombe ameyasema hayo wakati akitoa mada kwenye Mkutano Mkuu wa 34 wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT) nchini ulioanza leo katika ukumbi wa Jakaya Mrisho Kikwete jijini Dodoma uliowashirikisha Mameya, Wenyeviti na Wakurugenzi wa Halmashauri zote Nchini.
Mhandisi. Iyombe amewaagiza viongozi hao kuhakikisha wanajibu hoja za Mkaguzi Mkuu wa Serikali pamoja na maelekezo ya Kamati za Bunge kwa wakati ili kila Halmashauri iweze kupata hati safi.
“Serikali imekuwa ikitoa maagizo kuhusu kuhakikisha kila Halmashauri nchini inajibu hoja za Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali lakini bado kuna Halmashauri nyingi hazijafanya hivyo, naagiza tena kuwa kila Halmashauri kuacha kulimbikiza hoja za wakaguzi na zihakikishe zinajibiwa kwa wakati” Amesisitiza Mhandisi Iyombe.
Wakati huohuo amewataka viongozi hao kuhakikisha wanafanyakazi kwa ushirikiano na kuacha tabia ya kuwagawa watumishi kwa maslahi binafsi badala ya kuangalia maslahi ya jami jambo linalo kwamisha shughuli za jamii
“Ushirikiano mdogo kati ya Wakuu wa Wilaya,Mameya/Wenyeviti wa Halmshauri na Wakurugenzi unachangia kwa kiasi kikubwa kurudisha nyuma maendeleo katika Halmashauri nyingi nchini hivyo ni vyema wakafuata sheria na taratibu katika kufanya maamuzi katika utendaji kazi wao.
Ameendelea kufafanua kuwa kuna baadhi ya Halmashauri wanawagawa watumishi na kuleta majungu katika utendaji kazi wao jambo ambalo linasababisha kurudisha nyuma maendeleo katika Halmashauri na kushindwa kutoa huduma bora kwa jamii.
“Inasikitisha kukuta kuna watumishi wanaomsikiliza Meya/ Mwenyekiti na wengine kumsikiliza Mkurugenzi wa Halmashauri jambo hili si sahihi kwa kuwa huwezi kuongoza Halmashauri kama hakutakuwa na ushirikiano katika utendaji kazi’ Anasisitiza Iyombe
Hata hivyo amesisitiza kufuata sheria na taratibu katika kumuazimia mtumishi kwa kuwa upo utaratibu wa kufuata kama Mkurugenzi hatoshi kwenye nafasi yake kupunguza migogoro ya kiutumishi
Amewataka viongozi hao kuhakikisha wanasimamia Mapato na matumizi ya Halmashauri na kutoa nafasi kwa watumishi kwa kuwasikiliza kero zao lengo likiwa ni kujenga mahusiano mazuri katika utendaji kazi wao
“ Tengeni muda wa kuwasikiliza kero za watumishi na wananchi inasikitisha mtumishi anakuja mpaka Wizarani kufuatilia kero ambayo ingeweza kutatuliwa katika ngazi ya Halmashauri naagiza kero zote zitatuliwe katika ngazi ya Halmashauri.“Anasema Iyombe,
Aidha amewaonya Wakurugenzi kutokusita kuwachukulia hatua maafisa Mipango wote nchini wanaoshindwa kuandika maandiko ya miradi ya maendeleo ya kuzisaidia Halmashauri zao kwa ajili ya kuongeza vyanzo vya mapato.
Anaandika Angela Msimbira OR-TAMISEMI
Meatu, Simiyu, Tanzania
Anwani ya Posta: S.L.P 44
Simu: 028 2795 008
Simu ya Mkononi: 0622 404 712
Barua Pepe: ded@meatudc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Meatu . Haki Zote Zimehifadhiwa.