Benton Nollo, Meatu
Halmashauri ya Wilaya ya Meatu ni miongoni mwa Halmashauri 185 nchini zilizonufaika na ajira 16,676 ambazo zimetangazwa na Serikali leo tarehe 26 Juni 2022 ikiwa imepangiwa Watumishi 109 ambapo kati yao Watumishi wa Afya ni 58 na Walimu ni 51 (Elimu Sekondari Walimu 34 na Elimu Msingi ni Walimu 17).
Akizungumza na vyombo vya habari jijini Dodoma, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Innocent Bashunga (Mb) amesema katika kada ya afya Wataalamu 6,876 kati yao wanawake ni 3,217 sawa na asilimia 46.8 na wanaume 3,659 sawa na asilimia 53.2 waliomba na kukidhi vigezo wamepangiwa vituo vya kazi huku nafasi 736 za Madaktari wa Meno 59, Matabibu Meno 43, Matabibu Wasaidizi 244, Wateknolojia Mionzi 86 na Wauguzi ngazi ya Cheti 313 zikikosa waombaji wenye sifa.
Waziri Bashunga amebainisha kuwa kwa upande wa Kada ya Elimu, jumla ya walimu 9,800 waliokidhi vigezo wamepangiwa vituo vya kazi ambapo kati yao walimu 5,000 yaani wanawake wakiwa ni 2,353 sawa na asilimia 46.06 na wanaume 2,647 sawa na asilimia 57.94 wamepangiwa shule za Msingi na walimu 4,800 wanawake 1,289 sawa na asilimia 26.85 na wanaume 3,511 sawa na asilimia 73.15 wamepangwa shule za sekondari.
Ajira hizo ni jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Uongozi Mahiri wa Rais Samia Suluhu Hassan za kuhakikisha kila mtoto wa kitanzania anapata elimu bora ambapo Serikali imeendelea kutoa elimu bila malipo, imeboresha miundo mbinu ya kujifunza na kufundishia pamoja na kuendelea kulipa mishahara ya watumishi wa idara ya elimu huku ikiongeza idadi yao kwa kuajiri.
Vile vile, Serikali inahakikisha afya za Watanzania zinaimarika kwa kuboresha miundombinu ya sekta ya hiyo ambapo kwa upande wa Halmashauri ya Wilaya ya Meatu kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2021/2022 Serikali imetoa shilingi bilioni 1.64 kwa ajili ya ujenzi wa Vituo vya Afya vipya viwili ambavyo ni Kituo cha Afya Mwasengela (shilingi milioni 500) na Kituo cha Afya Iramba Ndogo (shilingi milioni 500) na majengo yanayojengwa katika vituo hivyo ni Jengo la Wagonjwa wa Nje – OPD, Maabara, Kichomea Taka, Wodi ya Wazazi na Upasuaji.
Katika Kituo cha Afya Bukundi Serikali ya Awamu ya Sita imeleta shilingi milioni 390 kwa ajili ya ujenzi wa Jengo la Wajawazito, Jengo la Upasuaji na Jengo la Maabara (shilingi milioni 300) ilhali shilingi milioni 90 zimeletwa kujenga Nyumba ya Watumishi (3 kwa 1) ambayo ujenzi wake tayari umeshaakamilika.
Kana kwamba haitoshi, Serikali pia imeleta shilingi milioni 250 kwa ajili ya ujenzi wa Jengo la Wagonjwa Mahututi – ICU katika Hospitali ya Wilaya ya Meatu na ujenzi wa jingo hilo upo katika hatua ya umaliziaji.
Pia, Serikali katika kuhakikisha afya za Watanzania zinaimarika wakiwemo wananchi wa Meatu imeendelea kutoa vifaa tiba na kulipa mishahara ya watumishi wa kada ya afya pamoja na kuajiri watumishi wapya kuanzia ngazi ya zahanati.
Aidha, kufuatia ajira za Watumishi zilizotangazwa tarehe 20 Aprili 2022, Watumishi wa Afya na Walimu 16,676 wamepangiwa vituo vya kazi kati ya Watumishi 17,412 waliotakiwa na nafasi 736 zimekosa waombaji wenye sifa hivyo zinatarajiwa kutangazwa tena.
Meatu, Simiyu, Tanzania
Anwani ya Posta: S.L.P 44
Simu: 028 2795 008
Simu ya Mkononi: 0622 404 712
Barua Pepe: ded@meatudc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Meatu . Haki Zote Zimehifadhiwa.