Na Benton Nollo, Isengwa
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Angellah Kairuki (Mb) amewapongeza wananchi wa Wilaya ya Meatu kwa mwamko walionao wa kujitolea nguvu kazi na kushiriki kikamilifu katika shughuli za utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Waziri Kairuki ameyasema hayo kwa nyakati tofauti wakati akikaguzi miradi ya elimu katika ziara yake ya siku moja aliyoifanya wilayani humo tarehe 26 Novemba 2022.
Akiwa katika Shule ya Sekondari Isengwa ambayo ni shule mpya ameupongeza uongozi wa mkoa, wilaya na Kamati ya Maendeleo ya Kata hiyo kwa kuwashirikisha Wananchi na wao wakahamasika kuchangia nguvu kazi hali ambayo imefanya miundombinu ya shule hiyo ikamilike na kupatiwa usajili.
“Binafsi niwapongeze kwa ushirikiano mlio nao kuanzia ngazi ya mkoa, wilaya, uongozi wa Kata hii ya Isengwa pamoja na Wananchi kwa ujumla…kwa kweli ninafarijika na ninafurahi sana ninapoona wananchi nao wanachangia maendeleo ya eneo lao…nchi yetu ni kubwa tukisema kila kitu kifanywe na Serikali hatutamaliza lakini mlivyoanza ndiyo maana Halmashauri nayo ikakamilisha madarasa hayo manne kupitia mapato ya ndani.” Amesema Kairuki na kuongeza;
“Tunawapongeza kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan na ndiyo maana naye ikampa nguvu kuweza kuwaletea madarasa mengine manne yenye thamani ya shilingi milioni 80…tusisite kuendelea kuwaangalia na kuwasimamia mafundi wetu ili madarasa haya yakamilike kwa viwango stahiki.”
Katika ziara hiyo Waziri Kairuki amelidhishwa na utekelezaji wa miradi katika shule alizotembelea na kumuagiza Mkuu wa Divisheni ya Miundombinu wilaya humo kusimamia maelekezo yote na ushauri uliotolewa na Mhandisi wa Mkoa wa Simiyu, Mhandisi Mashaka Luhamba kwamba mafundi wasimamiwe kwa kila hatua ya ujenzi ili majengo hayo yawe bora zaidi na kwa viwango stahiki.
Akiwa katika Wilaya ya Meatu, Waziri Kairuki amekagua ujenzi wa vyumba sita vya madarasa Shule ya Sekondari Mwandoya, vyumba vinne Shule ya Sekondari Kimali na vyumba vinne Shule ya Sekondari Isengwa.
Aidha, pamoja na ukaguzi huo pia Waziri Kairuki alitembelea na kukagua ujenzi wa Shule za Sekondari mbili mpya wilayani humo zinazojengwa kupitia Mradi wa Uboreshaji Elimu ya Sekondari – SEQUIP kwa gharama ya shilingi milioni 470 kila moja.
Kairuki hakuridhishwa na maendeleo ya ujenzi wa Shule ya Sekondari Mwanduitinje na kuiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) pamoja na Mkaguzi wa Ndani wa Halmashauri ya Wilaya ya Meatu kufanya uchunguzi na ukaguzi wa kina kwa kupitia nyaraka zote zinazohusika na ujenzi wa shule hiyo kwa kuilinganisha na Shule ya Sekondari Mwananimba ambayo kwa uhalisia pamoja na kwamba fedha zimeisha lakini majengo yake yamekamilika kwa ufanisi zaidi kuliko Mwanduitinje.
Pamoja na maagizo hayo Waziri Kairuki ametoa siku saba kwa Kamanda wa TAKUKURU Wilaya ya Meatu na Mkaguzi wa Ndani wa Halmashauri hiyo kukamilisha kazi hiyo na ripoti ya ukaguzi kwa shule hizo aipate haraka ofisini kwake.
“Mkaguzi wa Ndani wa Halmashauri na TAKUKURU tafadhali pitieni upya karatasi moja baada ya nyingine, mchoro wetu, nini kilitumika lakini na uhalisia wa mazingira ya eneo la Meatu sasa ili tutende haki…nikishaipata ripoti hiyo ndo ntajua tunatoa maelekezo ya aina gani, lakini nachotaka sisi kama Serikali hatuwezi tukaacha fedha Mheshimiwa Rais amezitoa majengo haya yakabaki hivi hivi…lakini kabla sijaelekeza chochote ebu tumalizane kwanza na TAKUKURU na Mkaguzi wa Ndani kila mmoja kwa namna yake…halafu tuweze kujua work schedule iliyobaki, materials yanayotakiwa ni kweli yanathibitika kwa milioni 264.” Amesema Kairukina kuongeza;
“Haiwezekani katika Halmashauri moja kuwe na utofauti mkubwa wa utekelezaji wa miradi hii, tena katika hali ya kusuasua, TAKUKURU fanyeni kazi yenu na Mkaguzi wa Ndani fanya kazi yako.”
Awali akitoa taarifa ya maendeleo ya ujenzi wa Shule ya Sekondari Mwanduitinje, Kaimu Mkuu wa Divisheni ya Miundombinu, Maendeleo ya Miji na Vijijini Wilaya ya Meatu, Mhandisi Joram Mwita amesema kwa sasa inahitajika shilingi milioni 264 ili kukamilisha ujenzi wa shule hiyo.
Halmashauri ya Wilaya ya Meatu kwa sasa inatekeleza ujenzi wa vyumba 74 vya madarasa katika shule za sekondari 21 baada ya kupokea shilingi bilioni 1.48 kutoka Serikali Kuu ikiwa ni maandalizi ya kuwapokea wanafunzi wa Kidato cha Kwsanza mwaka 2023.
Matukio katika Picha:
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Angellah Kairuki (Mb) akizungumza awali kabla ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa majengo ya Shule Mpya ya Sekondari ya Mwanduitinje inayojengwa kupitia Mradi wa Uboreshaji Elimu ya Sekondari – SEQUIP kwa gharama ya shilingi milioni 470 wakati wa ziara yake ya siku moja aliyoifanya wilayani Meatu, kukagua miradi ya elimu tarehe 26 Novemba 2022.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Angellah Kairuki (Mb) akikagua maendeleo ya ujenzi wa majengo ya Shule Mpya ya Sekondari ya Mwanduitinje inayojengwa kupitia Mradi wa Uboreshaji Elimu ya Sekondari – SEQUIP kwa gharama ya shilingi milioni 470 wakati wa ziara yake ya siku moja aliyoifanya wilayani Meatu, kukagua miradi ya elimu tarehe 26 Novemba 2022.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Angellah Kairuki (Mb) akizungumza awali kabla ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa majengo ya Shule Mpya ya Sekondari ya Mwamanimba inayojengwa kupitia Mradi wa Uboreshaji Elimu ya Sekondari – SEQUIP kwa gharama ya shilingi milioni 470 wakati wa ziara yake ya siku moja aliyoifanya wilayani Meatu, kukagua miradi ya elimu tarehe 26 Novemba 2022.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Angellah Kairuki (Mb) akikagua maendeleo ya ujenzi wa majengo ya Shule Mpya ya Sekondari ya Mwamanimba inayojengwa kupitia Mradi wa Uboreshaji Elimu ya Sekondari – SEQUIP kwa gharama ya shilingi milioni 470 wakati wa ziara yake ya siku moja aliyoifanya wilayani Meatu, kukagua miradi ya elimu tarehe 26 Novemba 2022.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Angellah Kairuki (Mb) akikagua maendeleo ya ujenzi wa vyumba sita vya madarasa ambavyo ujenzi wake unaendelea katika Shule ya Sekondari ya Mwandoya vinayojengwa kwa gharama ya shilingi milioni 120 ikiwa ni maandalizi wa kuwapokea wanfunzi wa Kidato cha Kwanza mwaka 2023, wakati wa ziara yake ya siku moja aliyoifanya wilayani Meatu, kukagua miradi ya elimu tarehe 26 Novemba 2022.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Angellah Kairuki (Mb) akikagua maendeleo ya ujenzi wa vyumba vinne vya madarasa ambavyo ujenzi wake unaendelea katika Shule ya Sekondari ya Kimali vinayojengwa kwa gharama ya shilingi milioni 80 ikiwa ni maandalizi wa kuwapokea wanfunzi wa Kidato cha Kwanza mwaka 2023, wakati wa ziara yake ya siku moja aliyoifanya wilayani Meatu, kukagua miradi ya elimu tarehe 26 Novemba 2022.
Meatu, Simiyu, Tanzania
Anwani ya Posta: S.L.P 44
Simu: 028 2795 008
Simu ya Mkononi: 0622 404 712
Barua Pepe: ded@meatudc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Meatu . Haki Zote Zimehifadhiwa.