Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amemuagiza Waziri wa Ujenzi, Mawasilianona Uchukuzi kutafuta Mkandarasi wa Ujenzi wa barabara za lami (kilomita tatu ) katika Mji wa Mwanhuzi wilayani Meatu Mkoani Simiyu.
Mhe. Rais Magufuli ameyasema hayo mapema jana wakati akiwahutubia wananchi katika Mkutano wa Hadhara uliofanyika katika Viwanja vya Stendi ya Mwanhuzi wilayani Itilima mkoani Simiyu, wakati akiwa katika ziara yake mkoani humo.
Amesema wakati akiwa Waziri wa ujenzi aliahidi ujenzi wa barabara hiyo Waziri wa ujenzi Mawasiliano na uchukuzi ahakikishe anamtafuta Mkandarasi ili aanze kufanya kazi hiyo mwezi huu Septemba 2018, ili ahadi hiyo aliyoitoa kwa wananchi wa Meatu itimie.
“Wakati nilipokuja hapa nikiwa Waziri wa Ujenzi niliahidi ujenzi wa kilomita tatu za lami, nimeshaangaa sana kuona hizo kilomita hazijajengwa, nakuagiaza Waziri wa Ujenzi kabla mwezi huu haujaisha nimuone mkandarasi anaanza kufanya kazi hapa” alisema
Aidha, Mhe. Rais amewataka wananchi kushirikiana na viongozi wao katika kujiletea maendeleo huku akiwasisitiza kuacha kujichukulia sheria mkononi na badala yake wazingatie sheria za nchi.
Katika hatua nyingine Mhe. Rais Magufuli amewaagiza Wakuu wa Mikoa na Wilaya kote nchini kushirikiana na Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuweka mipango itakayowezesha wakulima na wafugaji wanafanya shughuli zao kwa amani.
Awali akitoa salamu za Mkoa Mkuu wa mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka amesema mkoa huo una mpango wa kutambua na kuyapima maeneo ya Wafugaji na kuyawekea miundombinu ili wafugaji waachane na ufugaji waachane na kuhama hama na wafuge kwa tija.
Kwa upande wake Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi amesema Serikali inajiandaakufanya usanifu wa awali wa Ujenzi wa barabara ya Bariadi-Itilima-Kisesa-Mwandoya-Ng’oboko-Sibiti ili kwa baadaye ijengwe katika kiwango cha lami.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli anaendelea na ziara yake ya siku tatu mkoani Simiyu, ambapo Septemba 10 amesalimia wananchi katika maeneo mbalimbali ikiwemo Lagangabilili Itilima, Kisesa, Mwandoya, mkutano wa hadhara Mwanhuzi na kufungua majengo ya uboreshaji wa huduma za afya katika Hospitali ya Wilaya ya Meatu, kwa niaba ya vituo vingine 39.
Mwisho.
Meatu, Simiyu, Tanzania
Anwani ya Posta: S.L.P 44
Simu: 028 2795 008
Simu ya Mkononi: 0622 404 712
Barua Pepe: ded@meatudc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Meatu . Haki Zote Zimehifadhiwa.