OR TAMISEMI
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Mhe Innocent Bashungwa amesema katika mwaka wa fedha 2021/2022 Halmashauri 100 zimekusanya mapato ya ndani kwa asilimia 100 au zaidi ya lengo la mwaka.
Ameyasema hayo leo Agosti 2 , 2022 Jijini Dar-es-Salaam wakati akitoa taarifa kuhusu Mapato na Matumizi ya Ndani ya Halmashauri kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022.
Bashungwa amesema, Halmashauri 78 zimekusanya kati ya asilimia 80 hadi asilimia 99, na Halmashauri 7 zimekusanya kati ya asilimia 58 hadi 79. Halmashauri zilizofikia malengo ya mwaka zimeongezeka kutoka Halmashauri 57 katika mwaka wa fedha 2020/21, hadi kufikia Halmashauri 100 katika mwaka wa fedha 2021/22.
Amefafanua kuwa ulinganisho wa ufanisi wa ukusanyaji wa mapato ya ndani, kwa kigezo cha asilimia ya makusanyo, unaonesha kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha imeongoza katika Halmashauri zote kwa kukusanya asilimia 247 ya makisio yake ya mwaka, ikifuatiwa na Halmashauri za Wilaya ya Mlele asilimia 185, na Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro asilimia 158.
Vilevile, Waziri Bashungwa amesema , Halmashauri ya Wilaya ya Bumbuli imekuwa ya mwisho kwa kukusanya asilimia 58 ya makisio yake ya mwaka, ikifuatiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe asilimia 67, na Halmashauri ya Wilaya ya Bunda asilimia 70 ya makisio yake ya mwaka.
Ameendele kusema kuwa katika kuzipima Halmashauri zote kwa Kigezo cha wingi wa mapato (pato ghafi), jumla ya Halmashauri 35 zimekusanya zaidi ya Shilingi Bilioni 5. Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam imekusanya mapato mengi zaidi kuliko Halmashauri zote, kwa kukusanya Shilingi Bilioni 75.3 ikifuatiwa na Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni Shilingi Bilioni 47.3, na Halmashauri ya jiji la Dodoma Shilingi Bilioni 45.1.
Bashungwa amesema, Halmashauri 4 zimekusanya chini ya Shilingi Bilioni 1 ambapo Halmashauri ya Wilaya ya Bumbuli imekua ya mwisho kwa kukusanya Shilingi Milioni 599.7, ikifuatiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma Shilingi Milioni 692.1, Halmashauri ya Wilaya ya Madaba Shilingi Milioni 792.3, na Halmashauri ya Wilaya ya Buhigwe Shilingi Milioni 880.2.
Aidha, Halamashauri 4 zilizokusanya chini ya shilingi bilioni 1 zimeonekana kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa mapato. na haakuna Halmashauri iliyokusanya chini ya asilimia 50 kwa miaka yote miwili mfululizo
Meatu, Simiyu, Tanzania
Anwani ya Posta: S.L.P 44
Simu: 028 2795 008
Simu ya Mkononi: 0622 404 712
Barua Pepe: ded@meatudc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Meatu . Haki Zote Zimehifadhiwa.