Na Benton Nollo, Nyakabindi Bariadi
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Dkt. Yahaya Nawanda ametoa rai kwa wakazi wa mikoa ya Simiyu, Shinyanga na Mara kuweka akiba ya chakula ili kukabiliana na uhaba wa chakula kutokana na kutopata mvua za kutosha msimu wa mvua 2021/2022.
Dkt. Nawanda ametoa rai hiyo wakati wa kilele cha Maonesho ya Wakulima Nane Nane 2022 Kanda ya Ziwa Mashariki yaliyofanyika katika Viwanja vya Nyakabindi tarehe 08 Agosti 2022 ambapo alianza kwa kukagua baadhi ya mabanda ya maonesho na kisha kuzungumza na wananchi na kusisitiza kuweka akiba ya chakula.
“Katika Msimu wa Kilimo wa mwaka 2021/2022 hali ya uzalishaji wa mazao ya chakula haikuwa ya kuridhisha sana katika mikoa yetu hii mitatu, hivyo kuna uwezekano mkubwa wa kuwepo kwa uhaba mkubwa wa chakula kwa baadhi ya maeneo.” Amesema Dkt. Nawanda ambaye ndiye aliyekuwa Mgeni Rasmi na kuongeza:
“Kwa mantiki hiyo basi, naomba nitoe rai kwa wananchi wa mikoa hii mitatu, Simiyu, Mara pamoja na Shinyanga kuendelea kuchukua tahadhali ya kukabiliana na uhaba wa chakula unaoweza kujitokeza katika maeneo yetu…natoa rai kwenu wananchi kuhakikisha mnatumia chakula vizuri lakini msiuze chote ili muwe na akiba ya chakula cha mwaka mzima.”
Pia, Dkt. Nawanda amesema Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kuimarisha huduma za ugani kwa wakulima kwa kuwapatia vitendea kazi Maafisa Ugani wote nchini ili kuwafikia wakulima, wafugaji na wavuvi katika maeneo ya uzalishaji na kuwashauri kuhusu kilimo chenye tija na cha biashara.
Dkt. Nawanda amewahakikishia Wakulima kuwa Serikali kupitia Wizara ya Kilimo inaendelea kuwajengea uwezo Maafisa Ugani wote na kuwapatia mafunzo rejea na kuwaunganisha wakulima na maafisa hao kupitia Mfumo wa M-Kilimo ambapo Mkulima anaweza kuuliza maswali au kupata ushauri kuhusu kilimo, mifugo na uvuvi, sekta ambayo imeajiri zaidi ya asilimi 65.5 ya Watanzania wote.
Pamoja na mambo mengine, Dkt. Nawanda amewakumbusha wananchi kwamba maadhimisho ya Sikukuu ya Nane Nane mwaka 2022 yamebeba Kaulimbiu isemayo Ajenda 10/30 Kilimo ni Biashara, Shiriki Kuhesabiwa kwa Mipango Bora ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi.
Dkt. Nawanda amefafanua kwamba kaulimbiu hiyo inatoa ujumbe muhimu kwa Wakulima, Wafugaji, Wavuvi, Wanaushirika na Wadau wengine katika Sekta ya Kilimo ya kuboresha kilimo na kuongeza uzalishaji kibiashara na kuifanya nchi kuwa na ongezeko la kukua kwa uchumi na kufikia asilimia 10 ifikapo mwaka 2030.
Amesema, kwa kufanya hivyo nchi ya Tanzania itaweze kuuza bidhaa zake nje ya nchi kutoka dola za Kimarekani bilioni 5 hivi sasa na kufikia dola bilioni 12 ifikapo 2030.
Muhimu kabisa, Dkt. Nawanda amewakumbusha Wananchi kujitokeza kwa wingi kushiriki zoezi la Sensa ya Watu na Makazi ambalo litafanyika rasmi tarehe 23 Agosti 2022, zoezi ambalo litaifanya Serikali ya Tanzania kupata takwimu sahihi za watu na kuiwezesha kupanga mipango bora itakayosaidia kuinua uchumi wa Wakulima, Wafigaji na Wavuvi.
“Tunapaswa kuzingatia kuwa, ili Taifa letu liweze kupiga hatua kiuchumi, lazima tuanze kwa kuwabadilisha watu wetu kifikra, wafanye kazi kwa bidii na maarifa ili kila mmoja wetu aweze kuchangia maendeleo yake na taifa letu.” Amesema Dkt. Nawanda na kuongeza kwamba:
“Serikali yenu inatoa kipaumbele katika uzalishaji na upatikanaji wa malighafi ili kuwa na uhakika katika uendeshaji wa Viwanda vilivyopo na vinavyoendelea kuanzishwa.”
Naye Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Festo Kiswaga ambaye alimuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga amewasisitiza Wakulima kuendelea kutumia na kufuata kanuni bora za kilimo chini ya usimamizi wa Maafisa ugani wa kilimo ili kuifanya mikoa ya Simiyu, Shinyanga na Mara kuzalisha chakula cha kutosha.
“Zawadi ambayo tunaweza kumpa Rais Samia Suluhu Hassan sisi watu wa mikoa ya Shinyanga, Simiyu na Mara ni kuchapa kazi kwa bidii na kuzalisha chakula kwa wingi.” Amesema Kiswaga.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mara, Meja Jenerali Suleiman Mzee amewahimiza wananchi wa mikoa yote mitatu kwenda kuyafanyia kazi mambo yote mazuri ambayo wameyaona kwani Serikali inatumia fedha nyingi kuratibu maonesho hayo ili wananchi waweze kujifunza na wao kufanya kwa vitendo chini ya usimamizi wa wataalam.
Akizungumza awali, Mkurugenzi wa Kilimo kutoka Wizara ya Kilimo, Fares Mahuha amesema mpaka kufikia mwaka 2030 kilimo nchini kiwe kimefikia asilimia 10 na kazi ya kukifikisha kilimo katika ngazi hiyo ni lazima tushirikiane sote.
Halmashauri ya Wilaya ya Meatu mkoani Simiyu katika maonesho hayo yaliyoanza tarehe 01 Agosti 2022 hadi tarehe 08 Agosti 2022 imeibuka mshindi kwa kushika nafasi ya Kwanza katika Kundi la Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa mara ya tatu mfululizo.
Ambapo kwa mujibu wa taarifa iliyosoma na Mwenyekiti wa Kamati ya Uratibu wa Nane Nane Kanda ya Ziwa Mashariki, Beda Chamatata kupitia Kamati ya Ushindanishaji na Tathmini ya Maonesho ya Nane Nane 2022 ameeleza kwamba Halmashauri hiyo imepata alama 95.08 na kuzishinda Halmashauri zote 21 za Mikoa ya Simiyu, Shinyanga na Mara.
Halmashauri hizo zilishindanishwa katika maeneo matatu ambayo ni mabanda, vipando na mifugo ambapo wastani wa alama katika sehemu hizo ndiyo uliotumika kutoa mshindi wa kwanza hadi wa tatu.
Halmashauri nyingine zilizopata ushindi ni Halmashauri ya Manispaa ya Kahama mkoani Sinyanga ambayo imeshika nafasi ya pili na Halmashauri ya Mji Bariadi mkoani Simiyu ambayo imeshika nafasi ya tatu.
Mbali na ushindi huo, Halmashauri ya Wilaya ya Meatu pia imeshika nafasi ya pili katika mshindi wa jumla kwenye maonesho hayo yaliyofanyika kwenye viwanja wa Nyakabindi nje kidogo ya Mji wa Bariadi mkoani Simiyu.
Matukio Katika Picha:
Mgeni Rasmi katika Kilele cha Maadhimisho ya Sikukuu ya Wakulima Nane Nane 2022, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Dkt. Yahaya Nawanda (wa kwanza kushoto aliyevaa Skafu) na Mkuu wa Mkoa wa Mara, Meja Jenerali Suleiman Mzee (wa pili kushoto) kwa pamoja wakimkabidhi kombe Mkuu wa Divisheni ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi Wilaya ya Meatu, Thomas Shilabu (wa kwanza kulia) baada ya Halmashauri ya Wilaya ya Meatu kushika nafasi Kwanza katika Kundi la Mamlaka za Serikali za Mitaa kwenye Maonesho hayo yaliyoanza rasmi tarehe 01 Agosti 2022 na kuhitimishwa tarehe 08 Agosti 2022 yaliyofanyika katika Viwanja vya Nyakabindi nje kidogo ya Mji wa Bariadi mkoani Simiyu.
Meatu, Simiyu, Tanzania
Anwani ya Posta: S.L.P 44
Simu: 028 2795 008
Simu ya Mkononi: 0622 404 712
Barua Pepe: ded@meatudc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Meatu . Haki Zote Zimehifadhiwa.