Benton Nollo, Meatu
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Meatu, Dkt. Frank Mganga amesema kwa mwaka wa fedha 2021/2022 Halmashauri hiyo imekusanya shilingi bilioni 2.82 sawa na asilimia 110 ya bajeti kwa mwaka husika.
Dkt. Mganga ameyasema hayo leo tarehe 19 Julai 2022 alipokuwa akizungumza na Wajumbe wa Kamati ya Fedha, Uongozi na Mipango kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Musoma ambao wamefika katika Halmashauri hiyo kwa lengo la kujifunza mikakati inayotumiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Meatu kukusanya mapato hasa yale yanayotokana na zao la pamba.
Kaimu Mkurugenzi huyo amesema zao la pamba ndilo zao kuu na pekee la biashara linalotegemewa katika wilaya hiyo kwani takriban wakulima 44,000 hutegemea zao hilo na ni chanzo kikuu cha mapato ambapo zaidi ya asilimia 61 ya mapato yake kwa mwaka hutokana na ushuru wa zao la pamba.
Pia, Dkt. Mganga amesema Halmashauri ya Wilaya ya Meatu inatekeleza Mpango wa miaka mitano ulioanza msimu wa mwaka 2019/2021 na unatarajiwa kukamilika msimu wa mwaka 2023/2024, wenye lengo la kuongeza tija na uzalishaji kufikia tani 500,000 kwa Mkoa wa Simiyu na tani 150,000 kwa Wilaya ya Meatu.
Amesema ili kufikia malengo hayo Halmashauri hiyo inashirikiana na wadau wa Kampuni za ununuzi wa pamba kutoa michango ya fedha na vitendea kazi kwa lengo la kuwezesha uzalishaji wa pamba wenye tija.
Ambapo, kila kampuni ilitakiwa kutoa mchango wake wa shilingi milioni 10 na kwamba kampuni isiyotoa mchango huo haipewi kibali cha kununua pamba katika Wilaya ya Meatu, ambapo kwa mwaka wa fedha 2021/2022 shilingi milioni 102 zilipatikana kwa lengo la kutekeleza mpango huo.
Awali akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa mikakati ya uzalishaji wa zao la pamba na ukusanyaji wa ushuru wilayani Meatu kwa Wajumbe hao, Mkuu wa Divisheni ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Thomas Shilabu amesema mkakati wa kwanza ni uhamasishaji wa kilimo cha zao la pamba kwa wakulima kupitia mikutano ya vijiji kwa kutumia Wajumbe wa Kamati ya Mazao ya Wilaya, Kamati ya Uchumi na Hifadhi ya Mazingira wakishirikiana na Walezi wa Kata katika masuala ya kilimo.
Shilabu amesema mkakati wa pili ni kupitia mpango wa uchangiaji kwa lengo la kutekeleza mkakati wa kuongeza tija katika zao la pamba ambao Mkurugenzi Mtendaji ameueleza kwa kina.
Mkakati mwingine alioutaja Shilabu kwa wageni hao kuwa ni utoaji wa mafunzo ya mara kwa mara ya uzalishaji bora wa zao la pamba kwa wakulima kupitia mashamba darasa yanayosimamiwa na Wakulima Wawezeshaji 218 katika vijiji vyote 109 ambapo kila kijiji kina Wakulima Wawezeshaji wawili ambao wanasaidiana na Maafisa Ugani Kilimo waliopo.
Kadhalika, Shilabu amesema mkakati wa nne ni usimamizi wa shughuli za uzalishaji wa zao hilo kupitia vikosi kazi ngazi ya vijiji, kata na wilaya ambao kazi yao kubwa ni kusimamia na kuratibu shughuli za uzalishaji wa pamba katika hatua zote kuanzia uandaaji wa mashamba hadi uuzaji.
Shilabu ameongeza kwamba mkakati wa tano ni uhamasishaji wa kilimo cha zao hilo kwa wakulima kupitia mashamba ya viongozi wa Serikali ngazi ya wilaya ambapo kupitia mpango huo ekari 275 zililimwa.
Mbali na mikakati hiyo, Shilabu alieleza mikakati ya ununuzi na ukusanyaji wa ushuru wa pamba kuwa unalenga kuzuia utoroshaji wa pamba na udanganyifu wa taarifa za ununuzi wa pamba unaofanywa na makampuni ili kupata takwimu sahihi na hatimaye kupata mapato stahiki.
Shilabu aliitaja mikakati hiyo kuwa ni uundaji wa kikosi kazi cha usimamizi wa ununuzi wa pamba ngazi ya wilaya, uwekaji wa vizuizi vya pamba inayosafirishwa kutoka nje ya wilaya, kuweka masharti ya ununuzi na usafirishaji wa pamba ambapo kwa kampuni itakayobainika inatorosha pamba itatozwa faini ya shilingi milioni 5 au kufungiwa ununuzi wa pamba katika msimu husika au vyote kwa pamoja.
Sharti jingine alilolisema Shilabu ni kwamba, kampuni zote zinapaswa kununua pamba katika vituo stahiki vilivyoainishwa, hivyo kampuni hairuhusiwi kununua pamba shambani na kwenye kaya za wakulima na endapo kampuni itabainika kukiuka masharti hayo itatozwa faini ya shilingi milioni 3. Aidha, kampuni zilizopata kibali cha kununua pamba hutakiwa kulipia leseni ya biashara ya pamba kabla ya kuidhinishiwa kupata leseni Bodi ya Pamba.
Mtaalamu huyo amesema mkakati mwingine ni kuwawezesha Maafisa Ugani wa Kilimo kila kata na kijiji kusimamia shughuli za ukusanyaji wa ushuru wa pamba na kuchukua takwimu za manunuzi na masafirisho kwenye maeneo yao kila siku jioni na kuwasilisha taarifa hizo wilayani kila wiki.
Mkakati mwingine ni kuwawezesha wajumbe wa Kamati ya Mazao ya Wilaya pamoja na Kamati ya Uchumi na Hifadhi ya Mazingira kutembelea na kukagua vituo vya ununuzi wa pamba kwa lengo la kubaini na kuzuia mianya ya ukwepaji wa malipo ya ushuru kwa wanunuzi.
Shilabu amehitimisha kwa kuwaeleza wageni hao kwamba mkakati wa sita ni kutoa mafunzo kwa wajumbe wa Bodi wa Vyama vya Ushirika wa Mazao (AMCOS) ambapo wajumbe wa bodi 504 kutoka katika AMCOS 72 wamepatiwa mafunzo ya usimamizi na uendeshaji wa vyama vyao.
Pamoja na mambo mengine, Madiwani hao wamefurahishwa na namna Halmashauri ya Wilaya ya Meatu inavyodhibiti upotevu wa mapato katika vyanzo vyake na wametoa pongezi kwa namna ambavyo Halmashauri imefanikiwa kutoa shilingi milioni 354 ambayo ni asilimia 10 ya mapato yake ya ndani kwa Vikundi vya Wanawake, Vijana na Wenye Ulemavu kwa mwaka wa fedha 2021/2022.
Matukio katika Picha:
Mkuu wa Divisheni ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi Wilaya ya Meatu, Thomas Shilabu akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa mikakati ya uzalishaji wa zao la pamba na ukusanyaji wa ushuru wilayani Meatu kwa Wajumbe wa Kamati ya Fedha, Uongozi na Mipango kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Musoma ambao wamefika katika Halmashauri hiyo kwa lengo la kujifunza mikakati inayotumiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Meatu kukusanya mapato hasa yale yanayotokana na zao la pamba, ofisini kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo tarehe 19 Julai 2022.
Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Meatu, Christopher Ndamo akizungumza wakati akiwakaribisha Wajumbe wa Kamati ya Fedha, Uongozi na Mipango kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Musoma ambao wamefika katika Halmashauri hiyo kwa lengo la kujifunza mikakati inayotumiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Meatu kukusanya mapato hasa yale yanayotokana na zao la pamba.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Musoma, Charles Magoma akieleza madhumuni ya ziara yake na Wajumbe wa Kamati ya Fedha, Uongozi na Mipango kutoka katika Halmashauri yake ambao wamefika Halmashauri ya Wilaya ya Meatu kwa lengo la kujifunza mikakati inayotumiwa na Halmashauri hiyo katika ukusanyaji wa mapato hasa yale yanayotokana na zao la pamba, ofisini kwa Mkurugenzi Mtendaji tarehe 19 Julai 2022.
Mratibu wa Mapato katika Halmashauri ya Wilaya ya Meatu, Jesca Mnyare akieleza mbinu mbalimbali zinazotumiwa na Halmashauri hiyo kukusanya na kudhibiti upotevu wa mapato mbele ya Wajumbe wa Kamati ya Fedha, Uongozi na Mipango kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Musoma ambao wamefika katika Halmashauri hiyo kwa lengo la kujifunza mikakati inayotumiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Meatu kukusanya mapato hasa yale yanayotokana na zao la pamba, ofisini kwa Mkurugenzi Mtendaji tarehe 19 Julai 2022.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Musoma, Magange Mwita akizungumza wakati wa ziara yake na Wajumbe wa Kamati ya Fedha, Uongozi na Mipango kutoka katika Halmashauri hiyo ambao wamefika kwa lengo la kujifunza mikakati inayotumiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Meatu kukusanya mapato hasa yale yanayotokana na zao la pamba, ofisini kwa Mkurugenzi Mtendaji tarehe 19 Julai 2022.
Mkuu wa Kitengo cha Huduma za Sheria Halmashauri ya Wilaya ya Musoma, Nathan Mude akizungumza wakati wa ziara yake na Wajumbe wa Kamati ya Fedha, Uongozi na Mipango kutoka katika Halmashauri hiyo ambao wamefika kwa lengo la kujifunza mikakati inayotumiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Meatu kukusanya mapato hasa yale yanayotokana na zao la pamba, ofisini kwa Mkurugenzi Mtendaji tarehe 19 Julai 2022.
Matukio katika picha wakati wa ziara ya Wajumbe wa Kamati ya Fedha, Uongozi na Mipango kutoka katika Halmashauri ya Wilaya ya Musoma ambao wamefika kwa lengo la kujifunza mikakati inayotumiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Meatu kukusanya mapato hasa yale yanayotokana na zao la pamba, ofisini kwa Mkurugenzi Mtendaji tarehe 19 Julai 2022.
Meatu, Simiyu, Tanzania
Anwani ya Posta: S.L.P 44
Simu: 028 2795 008
Simu ya Mkononi: 0622 404 712
Barua Pepe: ded@meatudc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Meatu . Haki Zote Zimehifadhiwa.