Na Benton Nollo, Mwanhuzi
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Meatu, Msoleni Dakawa amesema Halmashauri hiyo kwa mwaka wa fedha 2021/2022 imepata mafanikio mbalimbali katika utekelezaji wa majukumu yake.
Dakawa ameyasema hayo wakati wa kikao cha Kamati ya Ushauri ya Wilaya ya Meatu - DCC kilichoketi kujadili taarifa ya mapitio ya utekelezaji wa Mpango na Bajeti kwa mwaka wa fedha 2021/2022, nusu mwaka wa fedha 2022/2023 na mapendekezo ya Rasimu ya Mpango na Bajeti ya mwaka wa fedha 2023/2024 kilichofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri ya Wilaya ya Meatu tarehe 24 Januari 2023.
Mkurugenzi huyo alisema mafanikio hayo yanatokana na dhamira ya dhati ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuboresha huduma za jamii na kukuza uchumi kwa Wananchi wake.
Dakawa ameyataja mafanikio hayo kuwa ni usajili wa Shule tano mpya za Sekondari ambazo ni Masalinge, Busangwa, Mwamanimba, Mwashata na Isengwa katika kata ambazo hazikuwa na Shule za Sekondari na hivyo kufanya wilaya kuwa na jumla ya Shule za Sekondari 29.
Pia, Dakawa amesema katika Wilaya ya Meatu Wanafunzi 3,583 (wavulana 1,599 na wasichana 1,974) wamesajiliwa kujiunga na Kidato cha Kwanza mwaka 2023.
Dakawa amesema kupitia Mpango wa Maendeleo na Ustawi wa Jamii dhidi ya Mapambano ya UVIKO 19 Halmashauri hiyo imejengwa madarasa 56.
Mbali na hayo, kupitia Mpango wa Kuboresha Elimu ya Sekondari - SEQUIP Serikali imeleta shilingi milioni 940 kwa ajili ya ujenzi wa Shule mbili mpya za Sekondari ambazo ni Mwamanimba na Mwanduitinje.
Kadhalika, Dakawa amesema katika kipindi hicho Halmashauri imepokea shilingi milioni 720 kwa ajili ya ukamilishaji wa vyumba 24 vya maabara, shilingi milioni 275 za ukamilishaji wa nyumba 22 vya madarasa ambazo ni fedha za tozo.
Milioni 100 ujenzi wa bweni moja, shilingi milioni 50 ujenzi wa nyumba wa watumishi 2 kwa 1 na shilingi milioni 135 ukamilishaji wa vyoo, madarasa na bweni ambazo ni fedha za mapato ya ndani.
DCC imeridhia na kupitisha Rasimu ya Mpango na Bajeti ya Halmashauri kwa mwaka wa fedha 2023/2024 ambapo imekadiria kukusanya na kutumia shilingi bilioni 39.97.
Kati ya fedha hizi Mapato ya Ndani ni shilingi bilioni 3.22 na kufanya ongezeko la asilimia 10 ukilinganisha na Bajeti ya mwaka 2022/2023 ambapo Bajeti ya Halmashauri ilikuwa shilingi bilioni 38.3.
Meatu, Simiyu, Tanzania
Anwani ya Posta: S.L.P 44
Simu: 028 2795 008
Simu ya Mkononi: 0622 404 712
Barua Pepe: ded@meatudc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Meatu . Haki Zote Zimehifadhiwa.