Na Benton Nollo, Mwanhuzi
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Meatu, Msoleni Dakawa amewahakikishia wananchi wa Mwanhuzi na Mwabuzo wilayani humo kuwa atahakikisha kila mwananchi aliyepemiwa ardhi anapatiwa Hati ya umiliki wa ardhi yake.
Dakawa ameyasema hayo kwenye Mkutano Maalum wa kuhamasisha Wananchi wa Vitongoji wa Ginnery, Jitobe na Mwasele vilivyopo katika Mji Mwanhuzi wilayani humo, kuchangia gharama za kupanga, kupima na kumilikishwa ardhi ambao ulifanyika kwenye viwanja vya Shule ya Msingi Mshikamano ‘A’ tarehe 19 Agosti 2022.
Alisema Halmashauri ya Wilaya ya Meatu kwa mwaka wa fedha 2021/2022 ilipokea shilingi milioni 93.5 kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa ajili ya upangaji, upimaji na urasimishaji ardhi nchini.
Dakawa aliainisha na kutaja wazi gharama za kupanga, kupima na kumilikisha ardhi kuwa ni shilingi 130,000.00 kwa kiwanja kimoja na hivyo kutoa wito kwa Wananchi kulipia gharama hizo ili waweze kupatiwa Hati za Umiliki.
“Ndugu zangu Serikali yetu imetuletea fedha shilingi milioni 93.5 ili tupange, tupime na tuweze kuwamilikisha ardhi… mpaka sasa hatua ya kwanza ya kupanga tulishamaliza, hatua ya pili ya kupima tulishamaliza hivyo hatua ya tatu ambayo ndiyo tupo nayo sasa ni ya kumilikisha.” Anasema Dakawa na Kuongeza:
“Tutahakikisha kila mwananchi aliyepimiwa ardhi yake anamilikishwa kwa kupatiwa Hati miliki…ndugu zangu hili siyo jambo dogo, Serikali yetu ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan inafanya mambo makubwa sana kwani gharama zilizotumika ni kubwa kwa mapato ya ndani ya Halmashauri tusingefanikiwa kwa wakati.
Dakawa aliwasihi wananchi hao kutumia fursa hiyo kulipia gharama hizo ili waweze kumiliki ardhi kisheria na kupatiwa hati ambazo zitawasaidia katika masuala mbalimbali ikiwemo taasisi za kifedha na kwa kufanya hivyo watakuwa wamejikwamua kiuchumi na kuinua kipato chao.
Akitoa taarifa ya upimaji wilayani humo Afisa Ardhi Mteule Wilaya ya Meatu, Rose Kinyamasongo alisema mradi huo unatekelezwa katika Kata mbili za Mwanhuzi na Mwabuzo ambapo tayari viwanja 2,000 (kila Kata viwanja 1,000) vimeshapimwa.
Kinyamasongo alisema zoezi la upangaji na upimaji limefanywa na Kampuni ya Makazi Solution kuanzia mwezi Januari 2022 na kukamilika Aprili 2022.
Matukio Katika Picha:
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Meatu, Msoleni Dakawa akizungumza kwenye Mkutano Maalum wa kuwahamasisha Wananchi tarehe 19 Agosti 2022 ambao ulifanyika kwenye Viwanja vya Shule ya Msingi Mshikamano 'A' na kujumuisha Vitongoji vya Ginnery, Jitobe na Mwasele mjini Mwanhuzi kuchangia gharama za kupanga, kupima na kumilikishwa ardhi (shilingi 130,000.00 kwa kila kiwanja) baada ya zoezi la upangaji na upimaji kukamilika. Zoezi la Upangaji na Upimaji lilifanywa na Kampuni ya Makazi Solution mwezi Januari hadi Aprili 2022.
Meatu, Simiyu, Tanzania
Anwani ya Posta: S.L.P 44
Simu: 028 2795 008
Simu ya Mkononi: 0622 404 712
Barua Pepe: ded@meatudc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Meatu . Haki Zote Zimehifadhiwa.