Na Benton Nollo, Mwanhuzi
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Meatu, Msoleni Dakawa amewapongeza Walimu kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kufundisha wanafunzi na usimamizi mzuri wa miradi inayopelekwa katika maeneo yao.
Dakawa ameyasema hayo wakati wa hafla fupi ya utiaji saini Mikataba ya Utendaji Kazi kati ya Mkuu wa Divisheni ya Elimu ya Awali na Msingi Wilaya ya Meatu, Elizabeth Kiraya pamoja na Mkuu wa Divisheni ya Elimu Sekondari Wilaya ya Meatu, Hadija Rajabu na Maafisa Elimu Kata wote 29 katika hafla fupi iliyofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri hiyo tarehe 13 Januari 2023.
Mkurugenzi Dakawa amesema pamoja na kwamba zipo changamoto mbalimbali ambazo zinawakabili walimu hao katika maeneo yao lakini ameeleza kuwa pamoja na yote hayo Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inaendelea kuzifanyia kazi.
"Madharani kwa mwaka huu wa fedha (2022/2023) Halmashauri yetu tumeletewa fedha zaidi ya shilingi milioni 980 kwa ajili ya kulipa madai (arrears) ya watumishi 750 kwa mara moja, hili siyo jambo dogo." Anasema Dakawa na kuongeza;
"Lakini pia katika mwaka huu huu wa fedha, Mheshimiwa Rais Sami ameridhia watumishi 499 kupandishwa vyeo...pia, katika miradi ya elimu tumeletewa shilingi bilioni 1.48 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa 74...kana kwamba haitoshi kupitia program ya EPforR tumeletewa shilingi milioni 190 katika Shule ya Sekondari Ngh'oboko...ndiyo maana nasema tuna kila sababu ya kumpongeza Rais wetu na sisi sote kwa kazi nzuri tunayofanya."
Aidha, Dakawa amewataka walimu na watumishi wengine wote katika Halmashauri hiyo kuepuka utoro kazini na kutokaa katika vituo vya kazi na badala yake wawajibike ipasavyo katika utekelezaji wa majukumu yao ili kuinua elimu na utoaji wa huduma bora kwa wananchi wa Meatu.
Pamoja na Maafisa Elimu Kata 29 waliohudhuria kusaini mikataba hiyo, kikao hicho pia kilihudhuriwa na Wakuu wa Shule 29 na Walimu Wakuu 122 wa Halmashauri ya Wilaya ya Meatu.
Meatu, Simiyu, Tanzania
Anwani ya Posta: S.L.P 44
Simu: 028 2795 008
Simu ya Mkononi: 0622 404 712
Barua Pepe: ded@meatudc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Meatu . Haki Zote Zimehifadhiwa.