Na Benton Nollo, Meatu.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Meatu, Msoleni Dakawa (pichani aliyevaa shati jeupe) tarehe 13 Mei 2022 ameongoza mamia ya waombolezaji wa Kijiji cha Ming'ongwa kwenye mazishi ya Njile Ngagaja (35) aliyefariki baada ya kukanyagwa na tembo waliovamia kijiji hichousiku wa kuamka tarehe 13 Mei 2022.
Mganga Mkuu wa Wilaya ya Meatu, Dkt. Frank Mganga amethibitisha kutokea kwa kifo cha mwananchi huyo wakati akipatiwa matibabu katika Kituo cha Afya Mwandoya alipofikishwa akiwa na hali mbaya baada ya kujeruhiwa vibaya na tembo huyo tumboni na miguuni.
Marehemu Ngagaja ni mkazi wa Kitongoji cha Ipililo, Kijiji cha Ming'ongwa Kata ya Sakasaka wilayani humo.
Tembo hao walivamia Kijiji hicho majira ya saa 4 usiku tarehe 12 Mei 2022 wakitokea Pori la Akiba la Maswa (Maswa Game Reserve) ambapo pamoja na kusababisha kifo kwa mwananchi huyo pia tembo hao wamesababisha taharuki na uharibifu mkubwa wa mali za wananchi ikiwemo mazao katika maeneo hayo.
Akitoa salamu za pole kwa familia, ndugu, jamaa na marafiki waliofiwa Dakawa amewasilisha salamu za Mbunge wa Jimbo la Kisesa wilayani humo, Luhaga Mpina kwa kuwaeleza kwamba amepokea kwa majonzi na masikitiko makubwa tukio la msiba huo na kuahidi kwamba kwa kuwa anaendelea na vikao vya Bunge la Bajeti jijini Dodoma ataonana na Waziri wa Maliasili na Utalii ili hatua mahususi na za haraka kudhibiti tembo hao na wanyama wengine waharibifu zichukuliwe.
Hata hivyo, Mbunge huyo baada ya kupatiwa taarifa hiyo ameshiriki kugharamia gharama za hospitali na mazishi ya mwananchi huyo.
Tatizo la wananchi kuvamiwa na tembo katika Wilaya ya Meatu hasa Jimbo la Kisesa, limekithiri licha ya kuwepo kwa jitihada mbalimbali zinazofanywa na Serikali kukabiliana na changamoto hiyo.
Hata hivyo, tarehe 04 Februari 2022 Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Simiyu, Shemsa Mohamed alifikisha kilio hicho mbele ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan katika Mji Mdogo wa Lamadi wilayani Busega akiwa njiani kuelekea mkoani Mara, ambapo Rais Samia aliiagiza Wizara ya Maliasili na Utalii kuanzisha vituo maalum vya kufukuza tembo katika vijiji vinavyopakana na hifadhi hiyo na kama hawana askari waombe kibali ili waongezewe askari.
Viongozi wengine waliohudhuria mazishi hayo ni Diwani wa Kata ya Sakasaka, Ofisi ya Mbunge Jimbo la Kisesa pamoja na Maafisa kutoka Pori la Akiba la Maswa.
Wananchi wa Vijiji 14 kati ya 18 vinavyopakana na Pori la Akiba la Maswa vipo Jimbo la Kisesa Wilaya ya Meatu mkoani Simiyu.
Vijiji hivyo ni Mbugayabhanya, Mwamashimba, Semu, Nyanza, Butuli, Sakasaka, Bulyandulu, Mwamhongo, Ng'hanga, Matale Ming'ongwa, Mwanindwa, Mwasengela na Tindabuligi.
Meatu, Simiyu, Tanzania
Anwani ya Posta: S.L.P 44
Simu: 028 2795 008
Simu ya Mkononi: 0622 404 712
Barua Pepe: ded@meatudc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Meatu . Haki Zote Zimehifadhiwa.