OR - TAMISEM, DODOMA.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Innocent Bashungwa (Mb) amesema katika bajeti ya mwaka wa fedha 2021/22 Serikali ilitoa shilingi bilioni 117 za Tozo za Miamala ya Simu kwa ajili ya ujenzi wa Vituo vya Afya 234 kwenye Tarafa na Kata ambazo hazikuwa na Vituo vya Afya.
Waziri Bashungwa ameyasema hayo Jijini Dodoma leo tarehe 01 Septemba, 2022 katika mkutano na vyombo vya habari kwa ajili ya kutoa ufafanuzi wa masuala ya tozo kwenye miamala ya Simu na benki ulioandaliwa na Wizara ya Fedha na Mipango.
Amesema kuwa ujenzi wa kila Kituo cha Afya umegharimu shilingi milioni 500 na umefanyika kwa upelekaji wa fedha kwa awamu 2, ambapo awamu ya kwanza zilipelekwa shiilingi milioni 250 na baadae shilingi milioni 250 kukamilisha.
”Haijapata kutokea tangu tupate uhuru, kujengwa Vituo 234 kwa wakati mmoja ndani ya mwaka mmoja wa fedha ambapo ujenzi ulihusisha majengo ya Wagonjwa wa Nje (OPD), Maabara, Jengo la Wodi ya Wazazi, Jengo la Upasuaji na Jengo kwa ajili ya Kufulia” amesema Bashungwa.
Ameendelea kufafanua kuwa Serikali imejenga miundombinu sambamba na ununuzi wa vifaa vya kisasa ambapo jumla ya shilingi bilioni 145.5 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba katika vituo hivyo 234 kwa ajili ya kuanza kutoa huduma kwa wananchi.
Pia amesema Serikali imeajiri watumishi wa Sekta ya afya 7612 kwa ajili ya kwenda kutoa huduma katika vituo hivyo vya kutolea huduma bora kwa wananchi.
Aidha, Bashungwa amesema katika sekta ya elimu, jumla ya Shilingi bilion 7 zimetolewa kusaidia ukamilishaji wa maboma 560 ili kupunguza mlundikano wa wanafunzi kwenye vyumba vya madarasa.
“Namshukuru sana Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa umahiri wake wa kuwajali wananchi wa Tanzania na kuwezesha miradi mikubwa kama hii.” Amesema Waziri Bashungwa.
Waziri Bashungwa amesema kuwa kwa upande wa elimu bila ada Serikali imehakikisha sera ya elimu bila ada katika mwaka wa fedha 2022/23 imetenga kiasi cha shilingi bilioni 346.5.
Vile vile, Waziri Bashungwa amewaagiza Wakuu wa Mikoa na Wilaya kuhakikisha wanasimamia utekelezaji wa miradi ambayo ilipokea fedha mwishoni mwa mwaka wa fedha 2021/22 na ikamilike kwa wakati ili kuanza kutoa huduma kwa wananchi ndani ya miezi minne baada ya kupokea fedha za ujenzi.
Meatu, Simiyu, Tanzania
Anwani ya Posta: S.L.P 44
Simu: 028 2795 008
Simu ya Mkononi: 0622 404 712
Barua Pepe: ded@meatudc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Meatu . Haki Zote Zimehifadhiwa.