Waziri wa Kilimo, Dkt. Charles Tizeba amewataka Waandaaji wa Maonesho ya Kilimo na Sherehe za Wakulima Nanenane hapa nchini kuhakikisha kuwa kuanzia mwaka 2019 wanaandaa maonesho hayo katika sura mpya itakayoleta mabadiliko chanya kwa wakulima, wafugaji na wavuvi ili waweze kuzalisha kwa tija.
Anaandika Stella Karinga - Simiyu.
Waziri Tizeba ameyasema hayo Agosti 03, 2018 katika Uwanja wa Nanenane Kanda ya Ziwa Mashariki, uliopo Nyakabindi Bariadi, wakati wa ufunguzi wa Maonesho ya Nanenane Kitaifa mwaka 2018 yanayofanyika Mkoani Simiyu.
Amesema ni vema waandaaji hao wakatoka katika maonesho ya mazoea ya kuwaonesha wakulima na wadau vipando mbalimbali pasipo kuwapa elimu ya namna yakufikia uzalishaji wanaouona katika maonesho, badala yake maonesho hayo yatumike kuwafundisha wananchi na kubadilishana uzoefu.
“Kuanzia nanenane ya mwaka huu na zinazofuata, wandaaji wazipe sura mpya hata tunapowaomba wadau mbalimbali kuchangia maandalizi wawe wananamini kuwa tutakachokifanya kitaleta mabadiliko chanya kwa wakulima, wafugaji na wavuvi wa nchi hii”alisema Tizaba.
Aidha, Dkt. Tizeba amekubaliana na mpango wa viongozi wa Mikoa ya Simiyu, Mara na Shinyanga kufanya maonesho kila baada ya miezi mitatu katika Uwanja wa Nyakabindi ili kuwapa fursa wananchi ya kuendelea kujifunza badala ya kusubiri kila wiki ya nanenane kila mwaka.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka amesema dhamira ya Mkoa huo na kanda ya Ziwa ya Mashariki ni kuendelea kufanya maonesho Teknojia za Kilimo Biashara katika Uwanja wa Nyakabindi jambo ambalo litawapunguzia Watanzania kwenda nje ya nchi kujifunza teknolojia hizo.
“Tutafanya maonesho hapa kila baada ya miezi mitatu, kupitia maonesho yatakayofanyika eneo hili, tutawapunguzia wananchi safari za kwenda nje ya nchi kufuata teknolojia za kilimo Biashara” alisema Mtaka.
Katika hatua nyingine Mtaka amesema Waoneshaji waliopo Uwanja wa Nanenane Nyakabindi wameomba kuongezewa siku mpaka kufikia Agosti 11 badala ya Agosti 08 kama ilivyo kawaida, jambo ambalo lilikubaliwa na Waziri wa Kilimo, Mhe. Dkt. Charles Tizeba.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Mara, Mhe. Adam Malima amesema matarajio ya viongozi wa Kanda ya Ziwa Mashariki ni kuyafanya maonesho ya nanenane kanda hiyo kuwa mnara wa mafanikio katika sayansi na teknolojia na namna ambavyo kilimo kinachozingatia kanuni bora kinavyochangia mabadiliko chanya ya mfumo wa Watanzania waanotegemea kilimo.
Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. Omary Mgumba ametoa wito kwa wananchi kufika Uwanja wa Maonesho ya Nanenane Nyakabindi ili kupata fursa ya kujifunza mambo mbalimbali kwa kuwa kwa sasa waoneshaji wa teknolojia mbalimbali wapo uwanjani hapo.
Maadhimisho ya Maonesho ya Kilimo na Sherehe za Wakulima Nanenane mwaka 2018 yanayofanyika Kitaifa Mkoani Simiyu ni ya 25 kufanyika hapa nchini na Waziri wa Kilimo Dkt. Charles Tizeba amesema maonesho hayo yatafanyika miaka mitatu mfululizo, mwaka 2018, mwaka 2019 na mwaka 2020.
Meatu, Simiyu, Tanzania
Anwani ya Posta: S.L.P 44
Simu: 028 2795 008
Simu ya Mkononi: 0622 404 712
Barua Pepe: ded@meatudc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Meatu . Haki Zote Zimehifadhiwa.