Mratibu wa mradi wa RMNCAH- UNFPA Idara ya Afya Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) Bi. Dinah Atinda amesema wahudumu wa ngazi za jamii wanajukumu kubwa la kutoa elimu, habari na unasuhi wa awali kwa wanawake wajawazito.
Ameyasema hayo wakati akifungua mafunzo ya siku saba kwa wahudumu wa afya ya Jamii Mkoani Simiyu inayohusu kuboresha afya ya Uzazi na Watoto wachanga ili kupunguza vifo vya mama na mtoto kwa wahudumu wa afya jamii Mkoani Simiyu.
Amesema kuwa ushirikishwaji wa jamii unatoa fursa kwa jamii kujihususha kufanya maamuzi yanayohusiana na afya zao na inaendeleza kufikia mikakati inayoweza kusaidia kupunguza kuchelewa kwa wanawake na familia zao kupata huduma za afya.
Amesema kuwa lengo la mafunzo hayo ni kuwapa elimu ili waweze kuisaidia jamii ambayo kwa sasa inaangamia kwa kukosa huduma bora za afya, kutokana na vifo vingi vya mama wajawazito na mtoto Mkoani Simiyu
Amesema kuwa wamama wajawazito wengi hujifungulia kwa wakunga wa jadi na kukosa huduma iliyo sahihi jambo ambalo linasababisha wakinamama wengi kufa kwa kukosa huduma za msingi za afya hivyo ni jukumu la watoa huduma ya afya ya jamii kuhakikisha wanatoa elimu kwa jamii juu ya umuhimu wa kujifungulia katika vituo vya afya.
Amesema takwimu zinaonyesha kuwa Mikoa ya Kanda yaziwa inaongoza kwa vifo vya mama na mtoto lakini Mkoa wa Simiyu unaidadi kubwa ya vifo vya Mama na Mtoto kwa asilimia 50 kutokana na mila potofu zilipo katika Mkoa huo
Amesema Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI ) kwa kushirikiana na wafadhili kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Ongezeko la Watu Duniani( UNFPA) wameboresha vituo vya afya na Zahanati ili viweze kuzalisha kinamama na kutoa huduma za upasuaji ndani ya vituo vilivyopo katika Halmashauri zao na kupunguza vifo vya mama na mtoto katika Mkoa huo.
Amesema Serikali kupitia shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Ongezeko la watu Duniani (UNFPA) wameweza kujenga imejenga vituo vya afya 38 vyenye uwezo wa kufanya upasuaji na zahanati ambazo zilikuwa hazina wodi za wazazi ziweze kuzalisha akina mama na majengo yakikamilika vitapatiwa vifaa ili huduma ya afya iwe nzuri kwa jamii.
Bi. Dinah amesisitiza kuwa Wahudumu wa afya ya jamii wanajukumu kubwa la kuelimisha jamii juu ya kuondokana na mila potofu, wakina mama kuudhuria Kiliniki na Zahanati zilizoko katika maeneo yao ili kupunguza vifo vya wamama wajawazito na watoto wachanga Mkoani Simiyu.