Mkoa wa Simiyu unatarajia kuvuna takribani tani 264,000 sawa na kilo milioni 264 hadi tani 490,000 sawa na kilo milioni 490 za zao la pamba, katika msimu wa mwaka 2017/2018 kutoka kilo milioni 70 za mwaka 2016/2017.
Hayo yamesemwa na Afisa Kilimo Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Ndg. Elias Kasuka katika Kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC) kilichofanyika Mjini Bariadi.
Kasuka amesema mkoa wa Simiyu una jumla ya wakulima wa pamba 301,000 watakaolima pamba katika msimu huu, katika eneo la zaidi ya ekari 700,000 huku matarajio ya mavuno yakiwa ni zaidi ya kilo 700 kwa ekari moja.
Mkuu wa Mkoa huo, mhe.Anthony Mtaka amesema Watalaam wa Kilimo wa Mkoa na Wilaya waandae mipango kazi yao itakayoonesha ratiba ya kuwatembelea wakulima wa pamba katika kipindi chote cha msimu tangu kupanda mpaka watakapovuna, ili malengo hayo ya kuongeza mavuno yaweze kutimia.
Mtaka ameongeza kuwa Zao la pamba linachangia kwa kiasi kikubwa mapato kwa Halmashauri za Mkoa huo, hivyo Wakurugenzi wanapaswa kuhakikisha Maafisa Kilimo wanawezeshwa muda wote wanaohitaji kuwafikia wakulima katika kipindi cha msimu wa kilimo badala ya kusubiri wakati wa ukusanyaji ushuru baada ya mavuno.
“Wakurugenzi nilishawaambia Uhai wa Halmashauri zenu uko kwenye ushuru wa pamba hakikisheni Maafisa Kilimo wanawezeshwa kuwafikia wakulima; Wakuu wa Wilaya pia kagueni mashamba ya pamba kwenye maeneo yenu. Wenyeviti wa Halmashauri niwaombe tusichangamkie pamba wakati inapovunwa tu, tuichangamkie hata pale inapokuwa shambani, tuwaone wananchi wanapolalamika kuwa mbegu hazijaoota au dawa hii haiuwi wadudu”alisisitiza Mtaka.
Meatu, Simiyu, Tanzania
Anwani ya Posta: S.L.P 44
Simu: 028 2795 008
Simu ya Mkononi: 0622 404 712
Barua Pepe: ded@meatudc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Meatu . Haki Zote Zimehifadhiwa.