Na Stella A. Kalinga
Mkoa wa Simiyu umejipanga kuandaa mwongozo wa uwekezaji kwa kila Kijiji na Mtaa utakaobainisha fursa za uwekezaji zilizopo katika kijiji na mtaa husika katika vijiji vyote 471 na Mitaa 92 ya wilaya zote tano za Mkoa huu, ikiwa ni maandalizi ya utekelezaji wa Falsafa ya Bidhaa Moja Kijiji Kimoja(OVOP) mwaka 2019/2020.
Hayo yamebainishwa Desemba 11, 2018 Mjini Bariadi katika kongamano la kuwajengea uwezo Watendaji wa Vijiji 471, Watendaji wa Mitaa 92, Watendaji wa Kata 130 na Maafisa tarafa 16 juu ya kuibua fursa za uwekezaji kwa ajili ya kuandaa mwongozo wa uwekezaji kwa kila kijiji na mtaa, kwa kushirikiana na Wataalam kutoka Taasisi ya Utafiti wa Masuala ya Kiuchumi na Kijamii (ESRF), ambalo pia limewahusisha viongozi na watendaji wa Chama na Serikali ngazi ya wilaya na Mkoa.
Awali akifungua kongamano hilo Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka amesema Mkoa huu unatekeleza Falsafa ya Bidhaa Moja Wilaya ambayo ilianza baada ya ESRF kufanya utafiti na kuibua fursa 26 ndani ya mkoa na sasa inajipanga kuandaa mwongozo wa uwekezaji kwa kila kijiji na kuanza utekelezaji wa Bidhaa Moja Kijiji Kimoja.
"Miaka mitatu ya utekelezaji wa Bidhaa Moja Wilaya Moja imetosha, mwaka 2019/2020 ni Bidhaa Moja Kijiji Kimoja, ESRF watatusaidia kufanya utafiti utakaoonesha kila kijiji kina fursa gani; Mkoa wa Simiyu utakuwa mkoa wa kwanza kwenye nchi hii ambao kila kijiji na mtaa utakuwa na mwongozo unaoonesha fursa za uwekezaji za kijiji au mtaa huo" alisisitiza.
Mtaka ameongeza kuwa mara baada ya kukamilisha mwongozo wa uwekezaji kwa kila kijiji, mkoa utaandaa utaratibu kwa kushirikiana na Shirika la Viwanda Vidogo (SIDO) kuona namna ya kuweka teknolojia/mashine zitakazotumika kuongeza thamani mazao ya kilimo, mifugo na mengine yanayopatikana katika kijiji au mtaa husika kulingana na fursa zitakazoainishwa.
Kwa upande wake Mtafiti Mkuu Mshiriki kutoka Taasisi ya Utafiti wa Masuala ya Kiuchumi na Kijamii(ESRF), Prof. Samwel Wangwe amesema mkoa wa Simiyu unafanya vizuri katika kilimo hivyo fursa za kuongeza thamani ya mazao ya kilimo zitakuwa kipaumbe cha kwanza, ikifuatiwa na uwekezaji kwenye miradi itakayoleta maendeleo ya binadamu pamoja na mageuzi katika masuala ya kijamii.
Nao Watendaji wa Vijiji, Mitaa na Kata wamewapongeza viongozi wa Mkoa kwa maono ya kila kijiji na mtaa kuwa na mwongozo wa uwekezaji na kuahidi kusimamia kikamilifu fursa zitakazoibuliwa katika maeneo yao, ili ziweze kuleta mapinduzi ya Kiuchumi kwa wakazi wa Simiyu.
" Nimeupokea vizuri sana mpango wa kila kijiji na mtaa kuwa na mwongozo wake wa uwekezaji, binafsi naahidi kusimamia kikamilifu fursa zote zitakazoibuliwa kupitia mafunzo tuliyopewa leo na tafiti zitakazofanywa na wataalam, ili zilete mapinduzi ya Kiuchumi kwa wananchi na mkoa wa Simiyu kwa ujumla" Twaibu Abdul Rashid, Afisa Mtendaji wa Kata ya Kinamweli wilaya ya Itilima.
"Tunamshukuru sana Mkuu wa Mkoa kuja na wazo hili ambalo tunaamini tukilisimamia vizuri litainua sana mkoa wetu kiuchumi, maana wananchi watakuwa wanafahamu kuwa ni eneo gani katika kijiji au mtaa wao linaloweza kuwainua kiuchumi kupitia uwekezaji watakapotambua fursa za uwekezaji zilizopo" Amina Yusuph Mtendaji wa Mtaa wa Ng'waswale, Halmashauri ya Mji wa Bariadi.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Simiyu, Mhe. Enock Yakobo amesisitiza kuwa ili kufikia malengo ya kuinua mkoa huo kiuchumi ni kuendeleza ushirikiano uliopo katika ya viongozi wa Chama na Serikali na wananchi.
MWISHO
Meatu, Simiyu, Tanzania
Anwani ya Posta: S.L.P 44
Simu: 028 2795 008
Simu ya Mkononi: 0622 404 712
Barua Pepe: ded@meatudc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Meatu . Haki Zote Zimehifadhiwa.