Mkuu wa Mkoa wa Simiyu,Mhe. Anthony Mtaka ameongoza Harambee ya Ujenzi wa Bweni la Wasichana katika Shule ya Sekondari Mwanjolo Wilayani Meatu ambapo jumla shilingi milioni 84,876,950/= zimepatikana, fedha taslimu ikiwa shilingi 18,776,000/= ahadi 66,100,000/= pamoja na mifuko 253 ya saruji, mbuzi 12 na ng’ombe 3.
Akizungumza na wananchi na viongozi wa Chama na Serikali Mtaka amewapongeza viongozi wa kata ya Mwanjolo kwa jitihada walizofanya kwa kushirikiana na wananchi katika kuhakikisha wanafunzi wa kike wanapata bweni, huku akiwasisitiza wananchi kuona umuhimu wa kuwekeza katika elimu ili kuuweka mkoa huo kwenye ushindani na mikoa mingine.
Aidha, ametoa wito kwa Madiwani wa kata zote mkoani humo kuiga mfano wa Kata ya Mwanjolo ambapo amesema viongozi na wananchi wanapaswa kuona uchungu na kuona haja ya kuwa na mabweni kwa watoto wa kike ili waondakane na vishawishi na changamoto nyingine zinazowakabili ili waweze kufikia malengo yao.
“Madiwani wetu hili jambo waige, haiwezekani hawa wasichana wadogo wanaenda kupanga kwenye vijiji pateni uchungu watoto wa kike wajengewe hosteli, Mungu ametupa ardhi, mifugo, nguvu za kufanya kazi, tukishikamana kama watu wa Mwanjolo, watoto wetu wa kike wote watapata mabweni”
“Mwanjolo wametuamasha, niwaombe waheshimiwa madiwani na viongozi wenzangu kwenye wilaya zote za Mkoa wa Simiyu moto huu uliowashwa hapa Mwanjolo uende kwenye kata zote, tuanze kujenga mabweni ya watoto wa kike wanapofaulu kwenda kidato cha kwanza wakae shule wasitembee njiani wakaanza kupewa lift za baiskeli na bodaboda” alisema Mtaka
Ameongeza kuwa kwa sababu elimu ni kipaumbe cha kwanza cha mkoa ni vema viongozi wote mkoani humo wakaweka dhamira kuwa kufikia mwaka 2020 wanafunzi wa kike wote wanaosoma shule za sekondari mkoani Simiyu wakae bweni.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Kisesa wilayani Meatu Mhe. Luhaga Mpina ametoa wito kwa Wananchi hususani jamii ya wafugaji kuchangia na kuunga mkono jitihada mbalimbali za maendeleo ya elimu ili watoto wa jamii za kifugaji waweze kusoma katika mazingira mazuri.
Wakati huo huo amewahimiza vijana wanaotoka katika jamii za kifugaji kusoma kwa bidii ili waweze kuzisaidia jamii zao kufuga ufugaji wenye tija utakaowaletea manufaa.
Nao wanafunzi wa kike wa Shule ya Sekondari Mwanjolo wamewashukuru viongozi na wananchi ambao wamechangia ujenzi wa bweni, ambapo wamesema endapo bweni hilo litakamilika litawasaidia kuondokana na vishawishi mbalimbali vilivyokuwa vikisababisha baadhi yao kupata ujauzito na kushindwa kumaliza masomo yao.
“Kukamilika kwa bweni kutatusaidia kutatua changamoto tunazokutana nazo sisi wasichana hasa suala la mimba, kuna wenzangu nilioanza nao kidato cha kwanza mwaka 2016 hawapo shuleni sasa hivi sababu ya mimba, naamini tukikaa bweni tutakuwa salama na tutapata muda mwingi wa kujisomea kwa kuwa hatutatembea mwendo mrefu tena” Eunice Kapombe mwanafunzi Kidato cha Tatu.
Kwa upande wao wazazi na walezi wa baadhi ya wanafunzi wa Shule ya Sekondari Mwanjolo wamesema ujenzi wa bweni la wasichana katika Shule ya Sekondari Mwanjolo utakuwa msaada mkubwa kwa watoto wa kike katika kuwawezesha kufikia kwenye malengo yao,kwa kuwa baadhi yao wamekuwa wakikatisha masomo kutokana na mimba zinazosababishwa na vishwawishi wanavyopata kwa kutembea mwendo mrefu kwenda shule na baadhi yao kupanga vijijini.
Harambee ya ujenzi wa Bweni la Wasichana Shule ya Sekondari Mwanjolo iliyofanyika Shuleni hapo Agosti 31, 2018, imehusisha viongozi wa Chama na Serikali ngazi ya Mkoa na Wilaya ya Meatu, Wadau mbalimbali wa Maendeleo na wananchi, ambapo mpaka kukamilika kwa Bweni hilo jumla ya shilingi 125,024,504.35 zitahitajika.
Meatu, Simiyu, Tanzania
Anwani ya Posta: S.L.P 44
Simu: 028 2795 008
Simu ya Mkononi: 0622 404 712
Barua Pepe: ded@meatudc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Meatu . Haki Zote Zimehifadhiwa.