Madiwani tisa kati ya 11 wa Halmashauri ya Wilaya ya Meatu waliojeruhiwa katika ajali iliyotokea Juni 10, 2018 kwenye msafara wa Mwenyekiti wa UVCCM Taifa, Mhe. Kheri James katika Kijiji cha Kisesa wilayani humo wametolewa katika Hospitali ya Rufaa Bugando baada ya kupatiwa matibabu ya awali na kusafirishwa kwenda Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa matibabu na uchunguzi zaidi.
Madiwani hawa walisafirishwa jana jioni wakisindikizwa na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Simiyu, ikiongozwa na Mkuu wa Mkoa huo, Mhe.Anthony Mtaka, viongozi wa CCM Mkoa wa Simiyu na viongozi wengine wa wilaya ya Meatu na Bariadi katika Uwanja wa Ndege wa Mwanza.
Wakizungumza kabla ya kuondoka Uwanja wa ndege wa Mwanza wametoa shukrani kwa madaktari na wauguzi waliowahudumia toka siku kwanza katika kituo cha Afya cha Mwandoya, Hospitali ya Wilaya ya Meatu, Hospitali Teule ya Mkoa wa Simiyu na Hospitali ya Rufaa ya Bugando kwa namna walivyowahudumia hali iliyochangia kuimarisha afya zao.
“Ninashukuru kwa matibabu ya awali niliyopewa Meatu na Bariadi yamenisadia sana, baada yaajali nilikuwa na maumivu makali sana lakini kutokana na huduma niliyoipata nina nafuu, yamebaki maumivu ya kifua kwa ndani” alisema Mhe. Pius Machungwa Diwani wa Kata ya Ngh’oboko ambaye pia Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Meatu.
“Katika ajali ile nilijeruhiwa sana maeneo ya mbavu, kiuno, miguu na mgongo nikawa siwezi hata kusimama lakini angalau sasa hivi naweza kusimama japo si kwa muda mrefu, nawashukuru sana watoa huduma wetu wa afya walijitahidi kutuhudumia” alisema Mhe. Consolata Lushu Diwani wa Viti Maalum Halmashauri ya Wilaya ya Meatu.
Katibu wa CCM mkoa wa Simiyu,Bw. Donald Magesa amesema jitihada kubwa zimefanyika katika kuokoa maisha yao tangu ajali ilipotokea na akawashukuru wote waliowahudumia kutoka Simiyu na Mwanza huku akiwawahakikishia kuwa Chama Cha Mapinduzi kitakuwa pamoja nao muda wote na wanawaombea madiwani wote wapone haraka.
Aidha, Magesa amesema Chama cha Mapinduzi kinaendelea kutoa pole kwa familia na ndugu wa Marehemu Mahega Masunga Selemani Diwani Kata ya Tindabuligi, ambaye alipoteza maisha katika ajali hiyo ambapo mwili wake unatarajiwa kuzikwa siku ya Jumatano nyumbani kwao Kijijini Zebea Wilayani Maswa.
Akizungumza kwa niaba ya Serikali ya Mkoa wa Simiyu, Mkuu wa Mkoa huo Mhe.Anthony Mtaka amemshukuru Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Luhaga Mpina ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Kisesa wilayani Meatu kwa kusaidia kukodi ndege maalum kwa ajili ya kuwasafirisha madiwani hao na akawatakia safari njema na kuwaombea heri ili wapone haraka na kurejea kwenye kazi ya kuwatumikia wananchi.
Mtaka pia amewashukuru madaktari waliowahudumia majeruhi wote tangu siku ya ajali Juni 10, wa kituo cha Afya Mwandoya, Hospitali ya Wilaya ya Meatu, Hospitali Teule ya Mkoa na Hospitali ya Rufaa Bugando ambapo amebainisha kuwa kwa hali iliyoripotiwa wakati wa ajali kama kungetokea uzembe wowote kwa madaktari watu wengi wangepoteza maisha, lakini kutokana na wepes wao wa kutoa huduma wamesaidia kuokoa maisha ya waliojeruhiwa
Wakati huo huo Mtaka ametoa pole kwa familia ya Marehemu Mahega Masunga Selemani Diwani Kata ya Tindabuligi ambaye alipoteza maisha katika ajali hiyo na kuwahakikishia kuwa Serikali ya Mkoa itashiriki katika mazishi ya diwani huyo na kueleza kuwa Uongozi wa Mkoa uko pamoja na familia na Baraza la Madiwani wa Wilaya ya Meatu katika wakati huu mgumu.
Waheshimiwa Madiwani waliosafirishwa kweda Muhimbili ni Pius Machungwa Diwani wa Kata ya Ngh’oboko na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Meatu, Emmanuel Mboje , Emmanuel Chalya, Seni Mizumale, Consolata Lushu, Juma Mpina, Chalya Igulu, Njile Ngwakwa, Mlangale Sakumi.na wengine wawili ambao ni Daudi Solo na Jeremia Kishola wamefanyiwa upasuaji Hospitali ya Rufaa Bugando na wapo katika vyumba vya uangalizi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Meatu, Ndg. Fabian Manoza Saidi(Kulia) akizungumza na baadhi ya Waheshimiwa madiwani waliojeruhiwa kwenye ajali ya Msafara wa Mweyekiti wa UVCCM Taifa, Kheri James kabla ya kuwasafirisha kwenda Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa ajili ya matibabu na uchunguzi zaidi.
Meatu, Simiyu, Tanzania
Anwani ya Posta: S.L.P 44
Simu: 028 2795 008
Simu ya Mkononi: 0622 404 712
Barua Pepe: ded@meatudc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Meatu . Haki Zote Zimehifadhiwa.