Na Linus R. James - MEATU DC
Mkuu wa wilaya ya Meatu Mh Dk. Joseph. E Chillongani mapema leo ameiongoza kamati ya Ulinzi na usalama ya wilaya ya Meatu, wakuu wa idara ya Halmashauri ya wilaya pamoja na taasisi na viongozi wa siasa katika ukaguzi wa maendeleo ya mradi wa ujenzi wa barabara mbali mbali za mitaa ya mji wa Mwanhuzi za kiwango cha lami zenye jumla ya Kilometa moja na nusu.
Mradi huu ni kati ya ahadi alizozitoa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 09 septemba 2018 katika viwanja vya Mwanhuzi wakati akiwahutubia wananchi alipotembelea Wilaya ya Meatu.
Kama ilivo ada ya kufanya vikao kabla ya kutembelea miradi mbali mbali Mkuu wa Wilaya alianza kikao hicho mapema asubuhi kwa kupokea taarifa fupi ya hali ya utekelezaji wa mradi kutoka kwa Meneja wa TARURA wilaya ya Meatu Mhandisi Mussa Miraji.
Meneja huyo alielezea kuwa mradi huu ni mkataba wa takribani Tshs Bilioni 2.4 ambao unajumuisha Maswa na Meatu lakini meneja huyo alisema anatoa taarifa ya hali ya utekelezaji kwa upande wa Meatu pekee.
Mhandisi huyo alisema Mradi ulianza utekelezaji wake tarehe 26 Novemba mwaka 2018 ambapo utachukua jumla ya miezi mitatu kukamilika ivyo unatarajiwa kukamilika ifikapo tarehe 24 Februari mwaka 2019.
Aidha alisema kuwa hali ya mradi ipo asilimia 60 na kazi zilizofanyika ni pamoja na kuweka vifusi na kuchimba mitaro ambapo kazi inaendelea.
Aidha alibainisha changamoto mbali mbali katika utekelezaji mradi ikiwa ni pamoja na mradi kuanza utekelezaji kipindi cha mvua, Wananchi kutokuheshimu alama za barabarani wakati wa ujenzi pamoja na mabomba kuwa ndani ya hifadhi ya barabara ambayo yamesababisha baadhi ya wananchi kukatiwa maji wakati wa utekelezaji wa mradi.
Pia Mhandisi huyo alikieleza kikao kuwa mradi huo licha ya kuwa unasimamiwa na TARURA wilaya, lakini kuna wasimamizi ngazi ya mkoa, na kitaifa ivyo aliwahakikishia kuwa barabara itakua ni ya hali ya ubora.
Baada ya kikao hicho Mkuu wa wilaya na timu yake walitembelea eneo lote la mradi na kujionea hali ya utekekelezaji ambapo alipata fursa ya kupata maelezo kutoka kwa Mkandarasi.
Akifanya majumuisho Mkuu wa Wilaya alisema kuwa hali ya mradi na ubora vinaridhisha.
“ Kuona ni kujifunza mengi Zaidi, lakini kuhusiana na ubora wenyewe , kwa jinsi wanavyomwaga vifusi ukilinganisha na barabara iliyopo utaona kuna utofauti , Tulitaka kuona ubora, kasi ya kazi pamoja na changamoto za mradi”. Alisema Dk. Chillongani.
Mwisho kamati ilitoa maagizo kwa mkandarasi na Meneja wa maji kuhakikisha kuwa sehemu ambapo mabomba yamekatika yarudishiwe haraka ili wananchi waendelee kupata huduma ya maji.
Ivyo mkandarasi alimuomba meneja wa Idara ya Maji apeleke mapendekezo ya gharama za vifaa ili aweze kupatiwa fedha anununue vifaa na alete mafundi kwa ajili ya kuunganisha mabomba ifikapo kesho.
MWISHO.
Meatu, Simiyu, Tanzania
Anwani ya Posta: S.L.P 44
Simu: 028 2795 008
Simu ya Mkononi: 0622 404 712
Barua Pepe: ded@meatudc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Meatu . Haki Zote Zimehifadhiwa.