Na Linus R. James
Wananchi ya Wilaya ya Meatu wamekumbwa na simanzi kubwa leo kutokana na ajali iliyotokea mapema leo majira ya saa tatu asubuhi maeneo ya Kisesa kilometa chache kutoka Wilaya ya Itilima.
Ajali hiyo imetokea wakati msafara wa mwenyekiti wa UVCCM Taifa ndugu Kheri James ukitokea Itilima kuelekea Meatu kwa ajiri ya ziara mbali mbali ikiwa ni pamoja na kukagua miradi na kusalimiana na wananchi pamoja na viongozi wa wilaya hiyo.
Akizungumza kwa njia ya simu Ndugu Hassan Hussein(Mabyelele) ambaye ni dereva wa Halmashauri ya Wilaya Meatu na ndiye alikua akiendesha gari lililowapakia waheshimiwa madiwani amesema gari la Halmashauri aina ya “Toyota Land Cruiser” lenye namba za usajiri STL 4981 limeharibika sana.
“Yaani ukiiona gari kwa nyuma haitamaniki, milango yote imevunjika, na ndo hiyo milango iliyombana Mheshimiwa mpaka akapata maumivu makali” Alisema Hassan
Baadhi ya Mashuuda mbali mbali waliokuwepo eneo la tukio wamesema chanzo cha ajali ni hitilafu iliyotokeaghafla (pancha) katika mojawapo ya gari lililokuwa mbele ya msafara na ivo kupelekea baadhi ya magari yaliyokua yanalifuata kupunguza mwendo . Hata ivo wakati magari yanapunguza mwendo, basi lenye namba za usajili T617CXN mali ya ROMBO EXPRESS lilishindwa kusimama ghafla na ivyo kuligonga gari lenye namba STL 4981 kwa nyuma na kusababisha taharuki.
Katika harakati za uokoaji kulitokea ajali ya pili iliyohusisha gari la kiongozi lililokuwa kwenye harakazi za uokoaji wa majeruhi yaani kuwakimbiza majeruhi hospitalini kwa ajiri ya huduma ya awali, katika ajali hiyo gari hilo lilimkosa kosa Mtu mmoja na kisha kugonga mti maeneo ya Isengwa.
Katika ajali hiyo jumla ya watu 20 walipata majeraha mbalimbali na kukimbizwa kwenye Hospitali ya Wilaya ya Meatu na Kituo cha Afya Mwandoya na kupatiwa matibabu ya awali.
Aidha, Majeruhi mmoja alifariki muda mfupi baada ya kufikishwa Hospitali ya Wilaya Meatu. Majeruhi aliyefariki anajulikana kwa jina la Mahega Masunga Selemani ambaye ni Diwani wa Kata ya Tindabuligi iliyopo Wilayani Meatu.
Majeruhi wengine kwenye ajali hiyo ni kama Mhe. Pius Z. Machungwa ambaye ni M/kiti wa Halmashauri Wengine ni Mhe. Juma I. Mpina, Mhe. Chalya Seni Igulu, Mhe. Daudi Matias Solo, Mhe. Seni Sita Mizumale, Mhe. Emmanuel Sayi Mboje, Mhe. Emmanuel Chalya, Mhe. Sasa G. Kishola, Mhe. Njile Ngwakwa, Mhe. Mlangale Sakumi, Mhe. Consolatha Lushu ambao wote ni Madiwani Kata mbali mbali Wilayani Meatu ambao baada ya kupata matibabu ya awali wamepata Rufaa Kwenda Hospitali ya Bugando Iliyopo koani Mwanza.
Wengine ni Ndg. Magreth Maneno, Ndg. Christina J. Hussein, Ndg. Daudi Masanja, Ndg. Bida Idaso, Ndg. Jeremiah Joseph, Ndg. Ngeleja Robert, Ndg. Philipo Malmala na Ndg.Christopher Mnanka ambao wengine wametibiwa na kuruhusiwa kurudi nyumbani aidha wengine wapo wanaendelea na matibabu hospitali ya Wilaya ya Meatu
Ofis ya mkurugenzi Mtendaji Wilaya ya Meatu imeunda kamati kwa ajilia kutekeleza majukumu ya kuainisha mahitaji ya kufanikisha shughuli ya mazishi ya Mheshimiwa huyo pamoja na kuainisha gharama za kuwasaidia majeruhi waliopata rufaa. Jumla ya shilingi 5,872,500.00 zimetengwa ili kukamilisha maandalizi ya mazishi pamoja na kutoa msaada wa awali kwa Majeruhi waliapata rufaa.
Hata hivyo, mchanganuo wa fedha hizo ni kuwa kiasi cha shilingi 2,000,000.00 kitatumika kuwasaidia majeruhi na kiasi cha shilingi 3,872,500 ni kwa ajili ya kukamilisha maandalizi ya shughuli ya Mazishi.
Mazishi ya Mhe. Mahega Masunga Selemani yanatarajiwa kufanyika tarehe 13.06.2018 nyumbani kijijini Zebea kilichopo Wilaya ya Maswa.
Mkurugenzi Mtendaji Ndugu Fabian Manoza anawapa pole ndugu, jamaa, marafiki wa wahanga wote waliokumbwa na tukio hili la kusikitisha. Aidha anawasihi wananchi wawe watulivu katika kipindi hiki kigumu na watumie mda huu kujumuika kumuombea marehemu na pia kuwaombea majeruhi wengine wapone haraka.
Meatu, Simiyu, Tanzania
Anwani ya Posta: S.L.P 44
Simu: 028 2795 008
Simu ya Mkononi: 0622 404 712
Barua Pepe: ded@meatudc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Meatu . Haki Zote Zimehifadhiwa.